Makamu wa Rais awataka wananchi kuwekeza katika elimu ya watoto wao

DODOMA-Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa watanzania kuwekeza katika elimu kwa watoto ikiwemo elimu ya dini kwa lengo la kukabiliana na mmomonyoko wa maadili unaolikabili Taifa hivi sasa.

Makamu wa Rais ametoa wito huo wakati akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Chemba akiwa katika siku ya tatu ya ziara yake ya kikazi mkoani Dodoma. Amesema ili Taifa liweze kupiga hatua za haraka linahitaji wananchi waliopata elimu.
Amesema kila mzazi na mlezi ni wajibu kusimamia na kuhakikisha watoto wanajengwa katika maadili mema kwa kupata mafundisho mazuri ya dini.

Halikadhalika Makamu wa Rais amesisitiza umuhimu wa kutunza mazingira ikiwemo kukomesha ukataji miti ovyo, kuacha kuchoma moto wakati wa kuandaa mashamba ya kilimo pamoja na uharibifu wa vyanzo vya maji.
Amesema athari ni kubwa zinazotokana na uharibifu wa mazingira ikiwemo kuanza kupata magonjwa, vifo vya Wanyama na binadamu, ongezeko la joto na ukosefu wa maji.

Amewahimiza viongozi kusimamia zoezi la upandaji miti hususani wakati mvua zitakapoanza na kusimamia miti hiyo kuhakikisha inafikia lengo.
Makamu wa Rais pia amesema Serikali ya Awamu ya Sita imedhamiria ifikapo mwaka 2034, asilimia 80 ya watanzania kutumia nishati safi ya kupikia.
Ameongeza kwamba serikali imedhamiria kuanzisha mfuko maalum ili kuweza kutoa ruzuku na kuwawezesha wananchi wa kawaida kutumia majiko ya gesi.

Amehimiza taasisi zinazolisha watu zaidi ya 100 kwa siku kuanza kutumia nishati safi ya kupikia kwa kuachana na ukataji miti kwaajili ya kuni na mkaa wa kupikia.
Amewasihi wananchi wa Wilaya ya Chemba kushiriki katika uchaguzi wa serikali za mitaa kwa kuzingatia kutunza amani iliyopo nchini.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiweka Jiwe la Msingi la akizindua Jengo la Ofisi ya Halmshauri ya Wilaya Chemba wakati akiwa ziarani mkoani Dodoma tarehe 21 Agosti 2024.

Awali Makamu wa Rais akiwa wilayani Chemba amezindua Mradi wa Jengo la Ofisi ya Halmshauri ya Wilaya Chemba ambao umegharimu shilingi Bilioni 4.6. amewataka watumishi kulitunza jengo hilo ili liweze kutumika kwa muda mrefu.

Mradi wa Jengo hilo unatarajiwa kurahisisha utoaji huduma kwa wananchi wa Wilaya hiyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news