Mamia kushiriki Wiki ya AZAKI 2024 jijini Arusha

DAR-Washiriki zaidi ya 500 kutoka Asasi za Kiraia (AZAKI), Sekta Binafsi, Serikali na wadau mbalimbali wa maendeleo wanatarajiwa kushiriki maadhimisho ya Wiki ya AZAKI 2024, itakayofanyika kuanzia Septemba 9 hadi 13,2024 jijini Arusha.
Mkurugenzi Mtendaji wa The Foundation for Civil Society (FCS), Justice Rutenge ameyasema hayo leo Agosti 23,2024 jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Amesema kuwa, wiki hiyo imebebwa na kauli mbiu ya Sauti, Dira na Thamani, ikiendana na wakati uliopo na matukio yanayoendelea nchini, ambayo ni pamoja na uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika mwaka huu, uchaguzi mkuu wa mwakani na Dira ya Taifa ya Maendeleo.

“Tupo kwenye kipindi muhimu sana kwenye demokrasia yetu kama nchi, kwa sababu mwaka huu tuna uchaguzi wa serikali za mitaa, wote mnafahamu.
"Pia mwakani tuna uchaguzi mkuu, lakini jambo la kipekee sana, mwakani tunatarajia kuzindua Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050 ambayo ni fursa adimu sana inayokuja mara moja kwa muda mrefu.

"Fursa hii kutokana na umuhimu wake ni budi sauti za wananchi zikasika kuchangia maoni yao wenye, kwani Dira ya Taifa inapaswa itokane na sauti, mawazo, mitazamo na maoni ya wananchi,"amesema Rutenge.
Aidha, Rutenge ameongeza kuwa, wiki hiyo pia itakuwa na mijadala mbalimbali inayohusu shughuli za AZAKI nchini, maendeleo ya jamii na ushirikiano baina ya Asasi za Kiraia, Serikali na sekta binafsi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Kimataifa linaloshughulika kusaidia na kuwezesha watu wenye ulemavu wa macho nchini (CBM), Nesia Mahenge ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Wiki ya AZAKi 2024 amesema kuwa, kuelekea katika wiki hiyo maandalizi yamekamilika, ambapo amewashukuru wadau wote waliojitokeza kudhamini na kuwezesha maadhimisho hayo.
Aidha, Mahenge ameeleza kuwa, katika wiki hiyo itayaleta pamoja makundi mbalimbali ikiwemo vijana, jamii, makundi maalum na wadau mbalimbali watakaojadiliana kwa pamoja mada zinazohusiana na kaulimbiu ya maadhimisho hayo.

Maadhimisho ya Wiki ya AZAKI 2024 ni ya sita kufanyika tangu kuanzishwa kwake mwaka 2018.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news