ZANZIBAR-Siku chache baada ya aliyewahi kuwa Msaidizi wa Maalim Seif Shariff Hamad na Juma Duni Haji,Ahmed Omar akiongozana na wanachama 368 kutoka vyama mbalimbali vya upinzani kuamua kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, mamia ya wapinzani wengine wameamua kufuata njia.
Waliojiunga na CCM Agosti 10,2024 katika Uwanja wa New Complex Amani wakati wa Uzinduzi wa Kampeni ya Kijana Kijani ya Tunazima zote Tunawasha Kijani walitoka katika Chama cha ACT Wazalendo na Chama cha Wananchi (CUF).
Aidha, wanachama hao walipokelewa na Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi.
Vile vile, Agosti 21,2024 Dkt.Mwinyi amewapokea wanachama 86 kutoka Chama cha ACT Wazalendo walioamua kujiunga na Chama Cha Mapinduzi katika Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Wanachama hao walifika katika mkutano ambapo, Dkt.Mwinyi alikuwa akizungumza na Wajumbe wa Kamati za Siasa za Halmashauri Kuu ya CCM ngazi ya Tawi, Wadi, Majimbo, Wilaya na Mkoa.
Aidha, leo Agosti 22,2024 Dkt.Mwinyi amewapokea wanachama 165 kutoka Chama cha ACT Wazalendo.
Vyama vingine ni Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Chama cha Wananchi (CUF) na ADC, ambao wameamua kujiunga na Chama Cha Mapinduzi.
Ni kupitia mkutano ambao umefanyika katika viwanja vya Tibirinzi, Mkoa wa Kusini Pemba, katika majumuisho ya mazungumzo na Wajumbe wa Kamati za Siasa za Halmashauri Kuu ya CCM ngazi ya Tawi, Wadi, Majimbo, Wilaya, na Mkoa.
Kwa nyakati tofauti wanachama hao wamemueleza mwandishi wa habari hizi kuwa,wameamua kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar bila kushurutishwa na mtu yeyote kwani ndani ya miaka karibia minne ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Nane chini ya Rais Dkt.Hussein Ali Mwinyi mambo ni mazuri.
"Licha ya kuwa kiongozi mcha Mungu, Mheshimiwa Rais Dkt.Hussein Ali Mwinyi ni mnyenyekevu kwa wananchi wote bila kujali hali zao za maisha.
"Umeshanifahamu, pia Dkt.Mwinyi ni kiongozi asiyependa dhuluma, mpenda haki. Ni kiongozi anayependa maendeleo ya watu, ndiyo maana unaona kila kona miradi inafanyika.
"Kwa hiyo, kiongozi wa namna ya Dkt.Hussein Ali Mwinyi kwa sasa hatunaye hata kule tulikotoka, ndiyo maana tumeona ni wakati sahihi kuungana naye ili kuhakikisha Zanzibar inapata maendeleo kila sekta."
Amesema, kwa sasa Zanzibar inapata maendeleo ya namna yake kutokana na miradi inayotekelezwa kuanzia ile ya kijamii, elimu, afya, miundombinu, kiuchumi na mingine.
"Ukitaka kuyajua anayofanya Rais Dkt.Mwinyi hapa Zanzibar njoo ukajionee mwenyewe, halafu linganisha na miaka kadhaa iliyopita, utapigwa na butwaa. Mambo ni mazuri mno."
Mwanachama mwingine aliyeamua kuamua kujiunga na CCM kutoka upinzani Zanzibar amesema, Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, Dkt.Hussein Ali Mwinyi amesema, Dkt.Mwinyi ni kiongozi mwenye sifa na vigezo vyote vya uongozi.
"Rais Dkt.Mwinyi ni kiongozi mwenye sifa za kipekee licha ya kuwa mpole, mvumilivu, mwadilifu, shupavu pia ni mtu wa watu.
"Pengine wengi hawajui kuwa ndiye kiongozi anayesikiliza kero za wananchi hata wale wa chini kabisa kuna mfumo wa Sema Na Rais (SNR), pale ukisema chochote kinamfikia mara moja na kinafanyikiwa kazi."
Amesema huku akisisitiza kuwa, sifa ya kiongozi bora ni mawasiliano na watu na hilo Rais Dkt.Mwinyi analifanya kupitia mfumo huo ikiwemo kuonana moja kwa moja na wananchi kupitia ziara na shughuli mbalimbali za kijamii.
Hata hivyo, wanachama hao wamebainisha kuwa, kutokana na kazi nzuri anazofanya Rais Dkt.Mwinyi wapinzani wengi siku si nyingi wataamua kuungana naye ili kuendeleza juhudi mbalimbali za kuwaletea wananchi wa Zanzibar maendeleo.