Mastercard yaunga mkono ushirikishwaji wa kifedha na ukuaji wa uchumi kupitia Jukwaa la Wadau Tanzania

DAR-Mastercard imeandaa jukwaa lake la kwanza la wadau nchini Tanzania lililofanyika jijini Dar es Salaam tarehe 14 Agosti 2024, na kuwakutanisha wadau muhimu katika tasnia ya teknolojia ya fedha.

Lengo ni kuangazia hali ya sekta na kukuza ushirikiano wenye matokeo chanya nchini.

Jukwaa hilo ni kielelezo cha dhamira ya Mastercard ya kuchangia katika ukuaji wa uchumi kupitia huduma bunifu za malipo ya kidijitali na ushirikiano wa kimkakati nchini Tanzania.
Rais wa Mastercard Afrika,Mark Elliott (kushoto),Dkt. Nkundwe Mwasaga, Mkurugenzi Mkuu, Tume ya Tehama (ICT), Elsie Wachira-Kaguru, Mkurugenzi, Msimamizi wa Biashara, Afrika Mashariki, Mastercard, Sadiki Nyanzowa, Kaimu Mkurugenzi wa Ustawi na Fedha Jumuishi, Benki Kuu ya Tanzania na Shehryar Ali, Makamu wa Rais Mwandamizi na Meneja wa Afrika Mashariki na Visiwa vya Bahari ya Hindi, Mastercard, wakiwa katika jukwaa la kwanza la wadau wa sekta ya fedha Tanzania lililoandaliwa na Mastercard.

Uchumi wa Tanzania umeonesha kuimarika, huku ukuaji halisi wa Pato la Taifa ukitarajiwa kufikia asilimia 5.7 mwaka 2024. 

Ripoti ya Benki ya Dunia inaonesha kuwa, licha ya changamoto za kiuchumi duniani, sekta ya huduma, hususan huduma za kifedha na bima, imekuwa na mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi nchini Tanzania.

Kampuni za teknolojia za kifedha zimeleta mageuzi kupitia huduma bunifu kama vile malipo kwa njia ya simu, uwekaji akiba kidijitali (mobile-wallets) na miamala ya blockchain, pamoja na kukuza wigo wa huduma za kifedha na kuwawezesha wananchi wasiofikiwa na huduma za kibenki. 

Ushirikiano baina ya Mastercard na wadau, sambamba na maendeleo ya teknolojia ni muhimu katika kufanikisha mageuzi hayo. Hii itahakikisha usalama na ufanisi katika huduma za malipo na kukuza mjumuisho wa kifedha na ushirikishwaji wa Watanzania katika uchumi.

"Jukwaa la Wadau Tanzania linaangazia dhamira ya Mastercard katika kuleta mageuzi ya kidijitali na uwezeshaji wa kiuchumi nchini Tanzania. Kwa kuwakutanisha wadau wa tasnia ya malipo na wabunifu.

"Tunatengeneza mazingira ya ushirikiano katika kutatua changamoto zilizopo, sambamba na kuweka mikakati ya kuhakikisha kuwa kila Mtanzania anapata huduma za kifedha kwa usalama na ufanisi. 

"Lengo letu ni kuimarisha teknolojia zetu na ushirikiano wa wadau wa ndani ili kuunda mfumo thabiti wa huduma za kifedha unaochochea ukuaji endelevu na ustawi kwa wote, "alisema Mark Elliott, Rais wa Mastercard Afrika.

Mkutano huo pia ulihudhuriwa na Sadiki Nyanzowa, Kaimu Mkurugenzi wa Ustawi na Fedha Jumuishi kutoka Benki Kuu ya Tanzania ambaye alisisitiza umuhimu wa mjumuisho wa kifedha na teknolojia mpya za malipo katika uchumi wa kidijitali ambao unaendelea kukua nchini.

Katika jukwaa hilo, jopo la wataalamu wakiwemo viongozi wa taasisi za sekta binafsi na viongozi wa serikali lilijadili mada kuhusu kuziba mapengo yaliyopo katika ushirikishwaji wa kifedha ili kufikia uwezeshaji wa kiuchumi. 

Jopo hilo lilijadili mchango wa teknolojia katika kupanua wigo wa upatikanaji wa huduma za kifedha. 

Mada zilizojadiliwa ni pamoja na mikakati ya kusaidia wajasiriamali, biashara ndogo na za kati (MSME), mipango ya pamoja, ubunifu katika huduma za kifedha kupitia simu za mkononi kwa jamii ambazo hazijafikiwa na huduma, na mifumo ya udhibiti katika kukuza ujumuishaji. 

Majadiliano hayo yalisisitiza umuhimu wa ushirikiano baina ya sekta ya umma na sekta binafsi, umuhimu wa teknolojia mpya kama vile blockchain na akili mnemba (Artificial Intelligence) katika kujenga uchumi jumuishi haswa kwa wanawake na vijana.

Jukwaa hilo lilihitimishwa kwa jopo lililojadili masuala ya usalama mtandaoni katika sekta ya malipo haswa kukabiliana na ulaghai mitandaoni. 

Majadiliano hayo yaliweza kubainisha sababu zinazochangia ongezeko la vitendo vya uhalifu wa taarifa ikiwemo uwekezaji na ujuzi mdogo pamoja na vihatarishi vya ndani. 

Aidha, washiriki walijadili nafasi ya akili mnemba katika usalama wa mitandao pamoja na kuangalia manufaa yake ukilinganisha na changamoto zinazoweza kujitokeza. 

Jopo pia liliangazia umuhimu wa mifumo ya zamani, masuala ya udhibiti, uhaba wa ujuzi na vikwazo vya kibajeti katika kujenga uchumi imara wa kidijitali.

Shehryar Ali, Makamu wa Rais Mwandamizi na Meneja wa Mastercard Afrika Mashariki na Visiwa vya Bahari ya Hindi alisisitiza umuhimu wa kukutanisha wadau katika jukwaa hilo ili kukuza ushirikiano na kuchangia katika maendeleo endelevu ya kiuchumi. 

"Jukwaa hili ni hatua muhimu katika kujenga mfumo imara na jumuishi wa kifedha nchini Tanzania. Kwa kutumia teknolojia za kisasa na kuendeleza ushirikiano wa kimkakati, malengo yetu ni kujenga mfumo-ikolojia wa malipo ulio salama na unaoweza kuzifikia jamii ambazo hazijafikiwa na huduma za kibenki kote barani Afrika,” alisema Ali.

Jukwaa la Wadau Tanzania lililoandaliwa na Mastercard ni sehemu ya mikakati ya Mastercard ya kujenga mfumo salama na jumuishi wa kifedha nchini Tanzania. 

Kupitia huduma bunifu za kidijitali na ushirikiano wa kimkakati na wadau wa ndani, Mastercard imejidhatiti kujenga mifumo ya malipo salama na inayoweza kuzifikia jamii ambazo hazijafikiwa na huduma za kibenki barani Afrika na kufanikisha dhamira yake ya kuwezesha watu bilioni moja kuingia katika uchumi wa kidijitali ifikapo 2025.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news