DODOMA-Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), Mhandisi Victor Seff ameelezea maeneo manne ya vipaumbele vya TARURA katika kusimamia ujenzi, ukarabati na matengenezo ya mtandao wa barabara za Wilaya nchini.
Mhandisi Seff aliyasema hayo wakati wa uwekaji jiwe la msingi wa ujenzi wa daraja la mto Hurui wilayani Kondoa mkoani Dodoma.
Alisema kuwa kipaumbele cha kwanza ni matengenezo ya miundombinu ya barabara ili kulinda uwekezaji ambao tayari umeshafanyika, ikiwa ni kuendelea na matengenezo hata pale barabara na madaraja yanapokamilika ili miundombinu hiyo iweze kudumu kwa muda mrefu.
Alieleza kuwa kipaumbele kingine ni kuondoa vikwazo kwenye mtandao wa barabara za Wilaya ili ziweze kupitika katika misimu yote ya mvua, mojawapo ya kazi ya kuondoa vikwazo ni pamoja na kujenga barabara kwa kutumia zege, kuweka makalavati na vivuko maeneo yote korofi ili hadi kufikia mwaka 2025/26 asilimia 85 ya mtandao wa barabara za Wilaya uweze kupitika nyakati zote.
"Mtandao wetu una zaidi ya Km. 144,000 lakini rasilimali fedha tunazopata bado ni kidogo, hivyo tunajitahidi kadri tunavyopata rasilimali fedha tunaondoa vikwazo ili barabara zetu ziweze kupitika nyakati zote,"alisema Mhandisi Seff.
Vile vile aliongeza kusema kuwa Wakala unatumia teknolojia mbadala pamoja na malighafi za ujenzi zinazopatikana maeneo ya kazi ikiwemo mawe katika ujenzi na matengenezo ya barabara kwa lengo la kuongeza ufanisi wa gharama, kupunguza muda wa utekelezaji na kutunza mazingira.
Pia, alisema wanazipandisha hadhi barabara kutoka udongo kuwa changarawe lakini kutoka changarawe au udongo na kuwa barabara za lami kwa kuzingatia vipaumbele vya kiuchumi na kijamii.
"Tunahudumia zaidi ya Km. 144,000 ya mtandao wa barabara lakini zaidi ya Km. 100,000 ni barabara za udongo, hizi ndio zina changamoto kubwa msimu wa mvua kwani maeneo mengi yanakuwa hayapitiki na kutokea taharuki ndio sababu tunajitahidi kadri rasilimali fedha tunazopata kuhakikisha kwamba tunaondoa vikwazo vyote ili barabara ziweze kupitika misimu yote ya mvua", aliongeza.