LINDI (Agosti 16, 2024)-Mahakama ya Wilaya ya Kilwa imemtia hatiani aliyekuwa Mhasibu wa Shirika la Msalaba Mwekundu Tanzania,Bw. Michael Kibaja katika Kesi ya Uhujumu Uchumi Namba 21225/2024.
Kibaja alikuwa anashtakiwa kwa makosa mwawili ambayo ni kughushi kinyume na Kifungu cha 333,335(a) na 337 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 Marejeo ya Mwaka 2022.
Sambamba na kosa la kutumia nyaraka kwa lengo la kumdanganya mwajiri Kinyume na Kifungu cha 22 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura ya 329, Marejeo ya mwaka 2022.
Mshtakiwa kati ya Februari 6,2020 na Machi 19, 2020 alighushi hati ya malipo ya Shirika la Msalaba Mwekundu Tanzania inayoonesha kwamba alimlipa mfanyakazi wa kujitolea kiasi cha shilingi 120,000 jambo ambalo halikuwa kweli.
Katika kosa la pili,mshtakiwa alitumia hati ya malipo iliyoghushiwa kwa kuambatisha katika fomu ya marejesho na kuwasilisha kwa mwajiri wake kwa lengo la kumdanganya kana kwamba alifanya malipo hayo.
Mshtakiwa aliomba kuingia makubaliano nje ya Mahakama (Plea Bargaining) na Mwendesha Mashtaka wa Serikali Wilaya ya Kilwa ambaye aliridhia kisha kuingia makubaliano hayo.
Wakati wa kusomewa mashtaka upya, alisomewa kosa moja kwa mujibu wa makubaliano ambalo ni kutumia nyaraka kwa lengo la kumdanganya mwajiri Kinyume na Kifungu cha 22 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura ya 329,Marejeo ya mwaka 2022.
Mshtakiwa alikiri kosa na kutiwa hatiani kisha kuhukumiwa kifungo jela mwaka mmoja au kulipa faini ya shilingi 500,000.
Aidha,Mahakama ilimtaka kulifidia Shirika la Msalaba Mwekundu Tanzania kiasi cha shilingi 500,000.
Mshtakiwa amelipa faini pamoja na kufidia Shirika kama ilivyoamriwa na Mahakama.
Kesi hii imeendeshwa na Mawakili wa Serikali Salum Bhoki na Gregory Chisauche, Mkoa wa Lindi.
Tags
Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania
Habari
Mahakamani Leo
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU)
TAKUKURU Tanzania