Mhasibu wa Shirika la Msalaba Mwekundu Tanzania afikishwa mahakamani kwa uhujumu uchumi

LINDI (Agosti 16, 2024)-aliyekuwa Mhasibu wa Shirika la Msalaba Mwekundu Tanzania, Bi.Carrie Chizara amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Kilwa na kusomewa mashtaka katika Kesi ya Uhujumu Uchumi Namba 21226/2024 .
Kwa mujibu wa Hati ya Mashtaka,Carrie Chizara anashtakiwa kwa makosa manne ambapo makosa mawili ni ya Kughushi kinyume na Kifungu cha 333, 335(a) na 337 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 Marejeo ya Mwaka 2022.

Aidha,makosa mengine mawili ni ya kutumia nyaraka kwa lengo la kumdanganya mwajiri Kinyume na Kifungu cha 22 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura ya 329, Marejeo ya mwaka 2022.

Katika makosa ya kughushi Mshtakiwa anadaiwa kati ya tarehe 18 Mei 2020 na tarehe 3 Juni 2020, alighushi Hati mbili za malipo za Shirika la Msalaba Mwekundu Tanzania.

Moja ikionesha aliwalipa wafanyakazi wawili wa kujitolea kiasi cha shilingi 300,000 kila mmoja na hati nyingine ikionesha amemlipa mfanyakazi mmoja wa kujitolea kiasi cha shilingi 300,000, jambo ambalo halikuwa kweli.

Makosa mawili ni ya kutumia nyaraka kwa lengo la kumdanganya mwajiri kinyume na Kifungu cha 22 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura ya 329, Marejeo ya mwaka 2022.

Pia, mshtakiwa anadaiwa alizitumia hati za malipo zilizoghushiwa kwa kuambatisha na fomu za marejesho na kuwasilisha kwa mwajiri wake kwa lengo la kumdanganya kana kwamba alifanya malipo hayo.

Mshtakiwa amekana mashtaka dhidi yake na ametimiza masharti ya dhamana.Kesi imepangwa kuja mahakamani kwa ajili ya kusomwa hoja za awali Septemba 26, 2024.

Kesi hii inaendeshwa na Mawakili wa Serikali, Salum Bhoki na Gregory Chisauche wa Mkoa wa Lindi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news