Mheshimiwa Sangu ataka watumishi walipwe mishahara kwa ufanisi wa kazi

DODOMA-Naibu Waziri, Ofisi ya Rais UTUMISHI na Utawala Bora Mhe. Deus Sangu amewataka viongozi wa Idara zote katika ofisi yake zinazohusika na uchakataji wa mishahara, kufanya utafiti wa kina kwenye taasisi za umma kuhusu utekelezaji wa majukumu ili mtumishi wa umma alipwe mshahara kutokana na ufanisi wa kazi.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais UTUMISHI na Utawala Bora Mhe. Deus Sangu akiuliza jambo Viongozi wa Idara ya Mishahara, Motisha na Marupurupu wakati wa kikao cha kumpitisha katika majukumu ya Idara hiyo kilichofanyika katika ukumbi mdogo wa Ofisi hiyo tarehe 13 Agosti, 2024.

Mhe. Sangu ameyasema hayo leo tarehe 13 Agosti, 2024 wakati alipokuwa akifuatilia mawasilisho mbalimbali ya majukumu ya Idara ya Mishahara, Motisha na Marupurupu, Idara ya Uendelezaji Rasimaliwatu, Idara ya Utawala wa Utumishi wa Umma na Idara ya Usimamizi wa Rasilimaliwatu Serikalini ikiwa ni sehemu ya kujifunza kuhusu majukumu ya Ofisi yake.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais UTUMISHI na Utawala Bora Mhe. Deus Sangu akifuatilia kwa makini mawasilisho ya majukumu ya Idara mbalimbali za ofisi yake wakati wa kikao chake cha kujifunza kilichofanyika katika ukumbi mdogo wa Ofisi hiyo tarehe 13 Agosti, 2024.

“Fanyeni utafiti wa mishahara Serikalini, kuna baadhi ya taasisi zilianzishwa na Serikali kwa nia njema ili kuboresha utoaji wa huduma na zikapewa mitaji na kufanya vizuri kwa muda mfupi na sasa hakuna wanachokizalisha lakini wanalipwa mishahara mikubwa inayoiongezea Serikali gharama za uendeshaji” alisema Mhe. Sangu.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais UTUMISHI na Utawala Bora Mhe. Deus Sangu akizungumza na viongozi wa Idara ya Uendelezaji Rasimaliwatu wakati wa kikao cha kumpitisha katika majukumu ya Idara hiyo kilichofanyika katika ukumbi mdogo ulipo jengo la Utumishi Jijini Dodoma leo tarehe 13 Agosti, 2024.

Hivyo, amezielekeza Idara hizo kufanya utafiti kwa taasisi za umma ili kubaini taasisi zenye mwenendo huo na matokeo ya utafiti yawasilishwe kwenye mamlaka yakiambatana na mapendekezo kwa hatua zaidi.

Vile vile, amesisitiza Idara ya Uendelezaji Rasilimaliwatu kufanya ufuatiliaji kwa Wizara na Taasisi za Umma ili kujiridhisha kama mwongozo wa mafunzo kwa watumishi wa umma unazingatiwa ipasavyo.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais UTUMISHI na Utawala Bora Mhe. Deus Sangu akifuatilia kwa makini mawasilisho ya majukumu ya Idara mbalimbali za ofisi yake wakati wa kikao chake cha kujifunza kilichofanyika katika ukumbi mdogo wa Ofisi hiyo tarehe 13 Agosti, 2024.

“Watumishi wanakaa ofisini bila kupewa mafunzo ya namna bora ya kutekeleza majukumu yao, hivyo kushindwa kuwa na uwezo wa kufanya kazi kwa ufanisi kwa sababu hawana ujuzi au ujuzi walionao umepitwa na wakati” amesema Mhe. Sangu.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais UTUMISHI na Utawala Bora Mhe. Deus Sangu akizungumza na viongozi wa Idara ya Utawala wa Utumishi wa Umma wakati wa kikao cha kumpitisha katika majukumu ya Idara hiyo kilichofanyika katika ukumbi mdogo ulipo jengo la Utumishi Jijini Dodoma leo tarehe 13 Agosti, 2024.

Hali kadhalika, ameongeza kuwa taaratibu za kufanya uchunguzi (vetting) kwa watumishi wanaotakiwa kushika wadhifa fulani ufanyike kwa haraka kwa kuwa kumpa nafasi au kumkaimisha mtumishi nafasi ya uongozi kwa muda mrefu na ikabainika kuwa hana sifa anaweza kuiweka Serikali kwenye matatizo.

Amepongeza kwa Idara ya Usimamizi wa Rasilimaliwatu Serikalini kwa kupata suluhu ya uchakataji wa mishahara kwa kutumia mfumo wa e-Watumishi na sasa mishahara inachakatwa ndani ya dakika 30 hadi saa moja tu badala ya siku 14 za hapo awali.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais UTUMISHI na Utawala Bora Mhe. Deus Sangu akizungumza na Viongozi wa Idara ya Usimamizi wa Rasilimaliwatu Serikalini wakati wa kikao cha kumpitisha katika majukumu ya Idara hiyo kilichofanyika katika ukumbi mdogo wa Ofisi hiyo.

Mhe. Sangu ameendelea na siku ya pili ya ratiba yake ya kujifunza kuhusu majukumu ya idara mbalimbali zilizopo katika ofisi yake yanayofanyika katika ukumbi mdogo wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mtumba Jijini Dodoma.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news