Mheshimiwa Sillo atoa maagizo kwa maafisa NIDA wa Kagera na Kigoma

KAGERA-Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mheshimiwa Daniel Sillo (Mb) amewataka maafisa wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) Mkoa wa Kagera na Kigoma kuhakikisha wanaharakisha utambuzi, usajili na usambazaji wa vitambulisho vya Taifa kwa wananchi.

Vitambulisho vya Taifa huwa vinatolewa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) ambayo ipo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani.
Mheshimiwa Sillo ameyasema hayo katika mkutano wa hadhara uliofanyika Agosti 10,2024 Bukoba Mjini ikiwa ni sehemu ya mwendelezo wa ziara ya siku sita ya Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM),Balozi Dkt.Emmanuel Nchimbi.

"Mheshimiwa Katibu Mkuu kote ulikopita kuanzia Kigoma Mjini, Kasulu, Ngara, Biharamulo, Kyerwa, Karagwe, Missenyi kule Kyaka huko kote umekutana na changamoto ya upatikanaji wa vitambulisho vya Taifa vinavyotolewa na NIDA."

Mheshimiwa Sillo amewaeleza wananchi ambao walikuwa katika mkutano huo kuwa kati ya mwaka 2021 na 2022 kulikuwa na tatizo la upatikanaji wa kadi ghafi kwa ajili ya kuzalisha kadi za vitambulisho vya Taifa.

"Lakini, Serikali sikivu ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan imetoa fedha bilioni 42.5 kwa ajili ya kuhakikisha kwamba kadi ghafi zinapatikana na wananchi wanapata vitambulisho vya Taifa.

"Na Mheshimiwa Katibu Mkuu kuanzia Oktoba 2023, tumeanza uzalishaji na usambazaji wa vitambulisho vya Taifa nchi nzima."
Naibu Waziri Sillo baada ya maelekezo hayo, ametoa maelezo kwa Afisa NIDA wa Mkoa wa Kagera, Afisa NIDA Mkoa wa Kigoma na maafisa NIDA wote wa Mkoa wa Kagera.

"Kuhakikisha kwamba wanaharakisha utambuzi na usajili, usambazaji wa vitambulisho vya Taifa kwa wananchi.

"Na washuke chini kule kwa wananchi, twendeni kwenye kata, twendeni kwenye mitaa, twendeni kwenye vijiji kuhakikisha kwamba wananchi wanapata vitambulisho vya Taifa."

Pia, amemueleza Katibu Mkuu huyo na wananchi kuwa, taarifa alizo nazo Mkoa wa Kagera kuna vitambulisho 78,766 ambavyo bado havijachukuliwa na wananchi.
"Niagize maafisa usajili NIDA wote kwenye wilaya zote kuhakikisha kwamba hizi kadi zote ambazo hazijachukuliwa zinachukuliwa na wale wanaostahili kuandikishwa wanaandikishwa ili wapate kadi hizi kwa ajli ya matumizi mbalimbali au mambo mbalimbali yanayohitajika maeneo mbalimbali."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news