NA GODFREY NNKO
MTO Ruvu umeendelea kuwa chanzo kikuu cha maji kwa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) ambapo wanapata asilimia 87 ya maji wanayozalisha.
Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), Mhandisi Mkama Bwire akiwasilisha wasilisho katika kikao kazi hicho leo Agosti 7,2024 jijini Dar es Salaam.
Vyanzo vingine ni visima asilimia saba, Mto Kizinga asilimia mbili na Mto Wami asilimia nne. DAWASA inatekeleza majukumu makuu mawili ikiwemo kutoa huduma ya maji safi na salama katika maeneo wanayohudumia na kusimamia usafi wa mazingira.
Hayo yamesemwa leo Agosti 7,2024 jijini Dar es Salaam na Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), Mhandisi Mkama Bwire.
Ni katika mwendelezo wa vikao kazi na wahariri wa vyombo vya habari nchini chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina (TR).
Amesema,bado kuna jitihada kubwa ambazo wanaendelea nazo kuhakikisha mtandao wa kilomita 7,087 wanaohudumia unakuwa na ufanisi mkubwa na kuleta matokeo chanya kwa wananchi na mamlaka kwa ujumla.
Mhandisi Bwire amesema, licha ya kutoa huduma mkoani Dar es Salaam pia wanatoa huduma baadhi ya maeneo Mkoa wa Tanga, Morogoro na Pwani.
"Katika kuboresha maeneo yetu ya huduma tumegawa mikoa ya kihuduma ya DAWASA takribani 23. Ilani inatutaka ifikapo 2025 tuwe tumefikia asilimia 95 ya huduma ya maji, lakini kwa sasa kwa mwelekeo wamefikia asilimia 93 kutokana na mtandao wa usambazaji maji.
Afisa Habari Mwandamizi kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina, Sabato Kosuri akiongoza kikao hicho leo Agosti 7,2024 jijini Dar es Salaam.
"Kazi kubwa tiliyo nayo ni kuangalia ni kwa namna gani haya maji yanawafikia wananchi."
Amesema, kuna maeneo ambayo yanapata maji muda wote, mengine kwa kiwango lakini mengine wapo katika hatua ya kufikisha huduma ya maji ili kuhakikisha wananchi wanafikiwa na huduma ya maji safi na salama.
"Ukienda maeneo ya Kigamboni kuna maji ya kutosha, kinachotakiwa ni kuongeza mtandao wa usambazaji vivyo hivyo kule Mkuranga na kwingineko."
Pia, amesema kutokana na vyanzo vya maji walivyo navyo kuonekana kuelemewa wapo mbioni kupata vyanzo vingine vya maji ikiwemo kutoka Mto Rufiji na Bwawa la Kidunda.
Mhandisi Bwire akizungumzia kuhusu Bwawa la Kidunda amesema, lengo la ujenzi wa bwawa hilo ni Klkuboresha upatikanaji wa huduma ya majisafi kwa wananchi kwa kuhakikisha maji katika Mto Ruvu yanapatikana kwa kipindi chote cha mwaka ili kutoa huduma ya majisafi kwa Mikoa ya Dar es Salaam, Kibaha na mji wa Bagamoyo.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano DAWASA, Everlasting Lyaro akitambulisha viongozi kutoka mamlaka hiyo leo Agosti 7,2024 jijini Dar es Salaam.
Pia, kuwezesha upatikanaji wa huduma ya majisafi kwa matumizi ya majumbani na viwandani, nishati ya umeme na baadaye wanaweza kuangalia namna ambavyo litasaidia katika kilimo cha umwagiliaji.
Ujenzi wa bwawa hilo ambao unatekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita unatarajia kutumia zaidi ya shilingi bilioni 300 na Mkandarasi ni Sino Hydro Corporation kutoka China ambaye tayari ameanza utekelezaji wake
Aidha, kukamilika Mradi wa Kidunda utawezesha mitambo ya Ruvu Juu na Ruvu Chini yenye kuzalisha jumla ya lita milioni 466 kwa siku, kuwa na uwezo wa kuzalisha maji katika majira yote ya mwaka na hivyo kuepusha upungufu wa maji katika majira ya kiangazi nchini.
DAWASA ni miongoni mwa taasisi na mashirika ya umma ambayo ipo chini ya Ofisi ya Msajili wa Hazina ambapo Septemba 2018, DAWASA na DAWASCO ziliunganishwa na kuendelea kufanya kazi na majukumu kama ilivyoainishwa katika Sheria ya DAWASA namba 20 ya Mwaka 2001.
Tags
DAWASA Tanzania
DAWASA YETU
Habari
Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF)
Ofisi ya Msajili wa Hazina