Mwanasheria Mkuu wa Serikali asisitiza uwajibikaji,weledi na ubora

DODOMA-Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Bw. Hamza Johari amewataka Menejimenti na Watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kufanya kazi kwa bidii huku wakiifuata na kuiishi kauli mbiu ya ofisi hiyo ya Weledi na Ubora.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali ameyasema hayo wakati alipokutana kwa mara ya kwanza na Menejimenti ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali mara baada ya kuwasili katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mtumba jijini Dodoma leo Agosti 19, 2024.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali aliambatana na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Bw. Samwel Maneno katika hafla hiyo fupi ya ukaribisho iliyofuatiwa na kikao na Menejimenti.
“Nawashukuru sana kwa mapokezi mazuri mlioyonipatia kwa kifupi niwasisitizie kuwajibika kwenye majukumu yetu ili tufikie malengo yetu kwa kufuata misingi ya weledi na ubora.”

Mwanasheria Mkuu wa Serikali ameahidi ushirikiano wa kutosha kwa Menejimenti na Watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika kufanikisha utelekezaji wa majukumu yao.
Kwa upande wake, Mhe. Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Bw. Samwel Maneno akizungumza wakati wa hafla ya kukaribishwa katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali alisisitiza wito wa kufanya kazi kwa bidii ili kuyafikia malengo ya ofisi hiyo.
“Ofisi yetu hii ina majukumu makubwa na mteja wake namba moja ni Serikali kwahiyo ili kufanikisha na kuifikia kauli mbiu yetu ya weledi na ubora kutatokana na ushirikiano baina yetu ninyi na sisi.”
Awali, akiwakaribisha Viongozi hao wapya katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali Jaji wa Mahakama ya Rufani Mhe. Jaji Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi amewapongeza Viongozi hao kwa kupata uteuzi huo na kuwaahidi ushirikiano kwenye masuala mbalimbali kila itakapohitajika.

Pia, ameitaka Menejimenti ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kuwapa ushirikiano Viongozi hao wapya walioingia katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
“Niwapongeze sana kwa kupata uteuzi huu, na nina imani mtaifanya Ofisi hii kuwa juu zaidi kwenye kuisaidia Serikali, hapa tuna timu nzuri ya Menejimenti niwaombe wajumbe wa Menejimenti kuwapa ushirikiano Viongozi hawa ili waweze kutekeleza majukumu yao vizuri na kwa ufanisi.

"Katika hatua nyingine aliyekuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ambaye sasa ni Mshauri wa Rais, Sheria na Mikataba Balozi Prof. Kennedy Gastorn akizungumza wakati wa hafla hiyo, aliwakaribisha Mwanasheria Mkuu na Naibu Mwanasheria Mkuu katika Ofisi huku akiiomba menejimenti ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuendelea kutoa ushirikiano kwa Viongozi wapya kama ambavyo walikuwa wakifanya chini ya uongozi uliopita.
”Kama ambavyo mlinipokea mimi na kunipa ushirikiano kwenye masuala mbalimbali basi nawaomba ushirikiano uleule muendeleze kwa kuwapatia Viongozi hawa wapya ili watekeleze majukumu yao.”
Naye Mwandishi Mkuu wa Sheria Bw. Onorius Njole, akizungumza kwa niaba ya Menejimenti ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, amewapongeza na kuwakaribisha viongozi wapya kwa kuajidi kuwa menejimenti itatoa ushirikiano na pia akiwashukuru na kuwatakia kila kheri kwenye majukumu yao mapya viongozi wanaondoka kwa utumishi wao ndani ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

“Kwa niaba ya Menejimenti ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali nawakaribisha sana Viongozi wetu wapya kwenye Ofisi hii na mimi na wenzagu tunawaahidi kuwapa ushirikiano wa kutosha wakati wa kutekeleza majukumu yenu.
"Pia nichukue nafasi hii kuwashukuru viongozi wetu mliomaliza muda wenu wa Utumishi kwenye Ofisi yetu na niwatakie kila la kheri kwenye majukumu yenu mapya yaliyoko mbele yenu”.

Baada ya kikao hicho Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali walikabidhiwa nyaraka na watangulizi wao, na kupata nafasi ya kutembelea Ofisi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news