Mwewe si saizi yake

NA LWAGA MWAMBANDE

ZINGATIA kuwa, shairi ni utungo wa kisanaa wenye mpangilio maalum wa lugha ya mkato unaowasilisha mawazo au ujumbe kuhusu mwanadamu au mazingira yake na hufuata utaratibu fulani.

Vile vile miongoni mwa lengo la shairi ni kupasha ujumbe kwa hadhira kwa njia ya upole na mvuto,kuelimisha na kuzindua jamii.

Pia,kuendeleza na kukuza kipawa cha utunzi,kuhifadhi msamiati wa lugha ya Kiswahili na sanaa ya fasihi,kuburudisha hadhira na wasomaji ikiwemo kuwasilisha hisia za ndani za mtu na mawazo.

Mshairi wa kisasa,Lwaga Mwambande licha ya kuendelea kuwasilisha ujumbe kwako kwa njia ya upole na mvuto wa namna yake, pia anaendelea kukupa elimu ambayo ni adimu kupitia tunzi zake za mashairi. Endelea kuelimika;

1. Kuku anabaki kuku, mwewe ni adui yake,
Hata awe na vikuku, mwewe si saizi yake,
Yeye chini ni shauku, mwewe anapaa zake,
Kushindanisha wawili, refa hatambulikani.

2. Kama refa yuko chini, rafu za mwewe si zake,
Hiyo mana yake nini, mwewe apeta kivyake,
Akiwa juu ya chini, yuko na jamaa yake,
Kushindanisha wawili, refa hatambulikani.

3. Nilivyowaona juzi, kuku na bata mwenzake,
Kwa mazoezi wajuzi, kila mtu na mwenzake,
Wasiwasi toka juzi, uwanja wa mechi yake,
Kushindanisha wawili, refa hatambulikani.

4. Kuku ni mkubwa kwake, wala sio mlo wake,
Ila vifaranga vyake, hivyo ni halali yake,
Kuku na kelele zake, mwewe vifaranga vyake,
Kushindanisha wawili, refa hatambulikani.

5. Kitaka teke la punda, uguse mkia wake,
Anaweza kukuponda, aridhishe roho yake,
Utabaki amekonda, ukiwa pembeni yake,
Kushindanisha wawili, refa hatambulikani.

6. Vifaranga vikiliwa, zabaki kelele zake,
Autangaze ukiwa, wausikie wenzake,
Apate kuhurumiwa, kirudi nyumbani kwake,
Kushindanisha wawili, refa hatambulikani.

7. Waingia mchezoni, wadai refa ni wake,
Wajidai ulingoni, ama zako ama zake,
Makali ya mkononi, mpini naona kwake,
Kushindanisha wawili, refa hatambulikani.

8. Damu meanza kutoka, mwewe anafanya yake,
Kiunzi utakivuka, uweze kufika kwake?
Au wataka sikika, yeye akipeta zake?
Kushindanisha wawili, refa hatambulikani.

9. Kuku mashindano yako, waweza uaibike,
Umalize pesa zako, wengine watajirike,
Bora ungelinda vyako, vifaranga siwe vyake,
Kushindanisha wawili, refa hatambulikani.

10. Pembeni ninasimama, kutazama mwisho wake,
Yule atayesimama, kipigwa filimbi yake,
Ninaombea salama, yakosekane mateke,
Kushindanisha wawili, refa hatambulikani.

11. Natamani kuwa mwewe, kule aliko nifike,
Kuku asiruhusiwe, nile vifaranga vyake,
Nani mgumu ka jiwe, asipende raha zake?
Kushindanisha wawili, refa hatambulikani.

12. Kama wakabiliana, kila mtu paso pake,
Vita yaweza umana, hakuna mshindi wake,
Hapo wakubaliana, kila mtu ale vyake,
Kushindanisha wawili, refa hatambulikani.

13. Refa bila kamisaa, tajifanyia kivyake,
Ni nani atamvaa, kuyapinga yale yake?
Tusubiri nusu saa, apige kipenga chake,
Kushindanisha wawili, refa hatambulikani.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news