ADDIS BABA-Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu -Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Patrobas Katambi ameshiriki katika Mkutano wa Umoja wa Afrika wa Kamati ya Kitaalam wa Mawaziri wa Afrika wanaoshughulikia masuala ya maendeleo ya jamii, kazi na ajira uliofanyika Agosti 1, 2024 jijini Addis Ababa, Ethiopia.Aidha, Mkutano huo hufanyika kila baada ya miaka miwili ambapo kwa mwaka huu 2024 mkutano huo umeongozwa na kauli mbiu isemayo, "Kudumisha Maendeleo Jumuishi katika Jamii yote.”
Katika mkutano huo, Mawaziri wameweza mujadili, kupitisha Sera, Mikakati na Matamko yanayolenga kuziwezesha nchi wanachama wa Umoja wa Afrika kutunga sheria sambamba na kutekeleza programu zenye lengo la kukuza ajira na kazi zenye staha kwa vijana pia kutoa kipaumbele kwa watu wenye ulemavu.
Vile vile, masuala mengine yaliyojadiliwa ni pamoja na kuweka mikakati thabiti ya kulinda haki za wafanyakazi wahamiaji, mikakati ya kutokomeza vitendo hatarishi kwa watoto na wanawake kama vile ndoa za utotoni na ukeketaji.
Pia, mkutano huo umepitisha matamko na mikakati yenye lengo la kuweka mazingira wezeshi kwa vijana na wazawa kupata fursa za kuajiriwa na kufanya kazi nje ya nchi katika kazi ambazo zina tija na maslahi kwao binafsi, nchi wanazokwenda na nchi yao kwa ujumla.
Mkutano huo umeudhuriwa pia na Naibu Waziri wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Mwanaidi Khamis pamoja na Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Zuhura Yunus Abdallah.