Naibu Waziri Sangu akerwa na tabia ya Maafisa Utumishi kutoa ushauri wa kuwafurahisha wakuu wao

NA LUSUNGU HELELA
Rukwa

NAIBU Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deus Sangu ameonya tabia ya baadhi ya Maafisa Utumishi na Maafisa Tawala kutoa ushauri kwa lengo la kuwafurahisha Wakuu wao badala ya kusimamia miongozo ya kazi zao hali inayopelekea ushauri huo kuwaumiza baadhi ya watumishi.
Amesema, tabia hiyo ya kujipendekeza imejengeka miongoni mwa Maafisa Utumishi na Maafisa Tawala hao ya kutaka kuonekana wao ni wema na wasiotaka kuwakwaza Wakuu wao muda wote.
Mhe. Sangu ametoa kauli hiyo leo kwenye Kikao kazi cha Watumishi wa Wilaya ya Sumbawanga mkoani Rukwa mara baada kusikiliza changamoto zinazowakabili na kuzitafutia ufumbuzi, ikiwa ni ziara ya kwanza kuzungumza na Watumishi tangu alipoteuliwa kushika wadhifa huo.

Amesema,tabia hiyo imewaumiza watumishi wengi kwani muda mwingi hutoa ushauri ambao ni kinyume cha haki na wajibu wa utumishi.
Katika hatua nyingine, Mhe. Sangu amezitaka Mamlaka za ajira na nidhamu kusimamia haki na stahiki zote za watumishi huku akizionya Mamlaka hizo kuacha tabia ya kufanya kazi kwa mazoea.

Amesema ni jambo la aibu kuona Watumishi waliostaafu wakianza kuhangaika kufuatilia taarifa zao ilhali kuna watu wanalipwa mshahara kwa ajili ya kazi hiyo.

Amesema kitendo cha watumishi wastaafu kuanza safari ya kuhangaika ya nenda rudi katika kufuatilia taarifa zao kana kwamba wao ndio waliojiajiri kinaleta taswira mbaya kuwa thamani na umuhimu wa mtumishi wa umma ipo tu pale ambapo mtumishi huyo akiwa bado hawajastaafu.
‘‘Jana nimekutana na mtumishi aliyestaafu miaka sita iliyopita akihangaika kufuatilia taarifa zake, nimeumizwa sana na kitendo hicho."

Kufuatia hatua hiyo, Mhe. Sangu ameagiza taarifa za watumishi ziandaliwe mapema ili anapofikia umri wa kustaafu ziwe zimekamilishwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news