Naibu Waziri Sangu apiga marufuku kuyatumia makundi haya kufanya kazi za TASAF

NA LUSUNGU HELELA
Rukwa

NAIBU Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na Mbunge wa Jimbo la Kwela, Mhe. Deus Sangu amepiga marufuku Walengwa wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) wakiwemo wazee wenye umri wa zaidi ya miaka 65, wenye ulemavu, akina mama wajawazito pamoja na watoto kufanya kazi za kujitolea huku akionya Watendaji watakaozembea kusimamia suala hilo hatua kali za kinidhamu zitachukuliwa dhidi yao.
Mhe. Sangu ametoa kauli hiyo leo kwa nyakati tofauti wakati akizungumza na Wananchi wa Kata ya Lusaka kwenye mikutano ya hadhara iliyofanyika kwenye vijiji vya Lowe, Lusaka, Kizumbi na Kamnyazya vilivyopo Jimbo la Kwela, Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga Mkoani Rukwa, Ikiwa ni ziara yake ya kwanza tangu alipoteuliwa kushika wadhifa huo.
Amezitaja kazi hizo za kujitolea ambazo huratibiwa na TASAF kuwa ni ulimaji wa barabara pamoja na uchimbuaji wa mitalo ya barabara.

Amesema,kundi hilo lisisumbuliwe kufanya kazi hizo kwani sio sawa kutokana na hali zao.

Katika hatua nyingine Mhe. Sangu amezitaka Kaya zinazonufaika na Mpango wa TASAF kuhakikisha kama zina wanafunzi waliohitimu kidato cha sita na wanatarajia kujiunga Chuo Kikuu wawasilishe majina yao katika Ofisi za Halmashauri zao ili waweze kupata kipaumbele cha kupata mkopo kutoka Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu utakaowawezesha kuendelea na masomo ya Chuo Kikuu kwani Bodi hiyo imeingia mkataba na TASAF.
Amesema, lengo la TASAF kuingia mkataba na Bodi ya Mikopo wa Elimu ya Juu ni kuhakikisha watoto wanaotoka katika Kaya maskini hawakosi mkopo ili kuhakikisha wanafaulu ili badae waweze kurudi kwa ajili ya kuzikomboa Kaya zao kwenye lindi la umaskini.

Amesema ni jambo lisilokubalika chini ya Uongozi makini wa Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuona Mtoto aliyetoka kwenye kaya maskini kasoma na wazazi wake ni wanufaika wa TASAF lakini anakosa mkopo anapotaka kujiunga Chuo Kikuu.
Kufuatia hatua hiyo Mhe.Sangu amewaagiza Waratibu wa TASAF wa Mikoa pamoja na Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri zote nchini kuhakikisha wana wasaidia watoto hao ili waweze kutimiza ndoto zao.
Aidha, Mhe.Sangu amezitaka Kaya zenye watoto ambao ni Walengwa wa Mpango wa TASAF lakini Watoto hao hawajabahatika kujiunga kidato cha kwanza wachangamkie fursa ya ufadhili wa masomo unatolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu kujiunga VETA.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news