NBS:Mfumuko wa Bei umepungua hadi asilimia 3.0 kutoka asilimia 3.1

NA GODFREY NNKO

OFISI ya Taifa ya Takwimu (NBS) imesema, Mfumuko wa Bei wa Taifa kwa mwaka ulioishia mwezi Julai, 2024 umepungua hadi asilimia 3.0 kutoka asilimia 3.1 kwa mwaka ulioishia mwezi Juni, 2024.
Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt. Albina Chuwa.(Picha na Maktaba).

Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Agosti 9,2024 na Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt.Albina Chuwa.

"Hii inamaanisha kuwa, kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia mwezi Julai, 2024 imepungua ikilinganishwa na kasi iliyokuwepo kwa mwaka ulioishia mwezi Juni, 2024.

"Kupungua kwa kasi ya Mfumuko wa Bei kwa mwaka ulioishia mwezi Julai, 2024 kumechangiwa na kupungua kwa Mfumuko wa Bei wa baadhi ya bidhaa zisizo za chakula."

NBS imepewa mamlaka kwa mujibu wa Sheria ya Takwimu Sura 351 ya kutoa, kusimamia na kuratibu upatikanaji na usambazaji wa Takwimu Rasmi nchini ikiwa ni pamoja na takwimu za Mfumuko wa Bei kwa ajili ya matumizi ya Serikali na wadau wa takwimu.

Aidha,Mfumuko wa Bei wa Taifa unapima kiwango cha kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma zote zinazotumiwa na kaya binafsi nchini.

Dkt.Chuwa amesema,baadhi ya bidhaa zisizo za chakula zilizoonesha kupungua kwa Mfumuko wa Bei kwa mwaka ulioishia mwezi Julai 2024 ikilinganishwa na mwaka ulioishia mwezi Juni, 2024 ni pamoja na vitambaa vya kushona nguo kutoka asilimia 1.6 hadi 1.3.

Nyingine ni bidhaa kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa jengo kutoka asilimia 3.1 hadi
1.6, mkaa kutoka asilimia 29.3 hadi 28.4.

Vilevile, samani za nyumbani kutoka asilimia 4.7 hadi 4.5 na mazulia kutoka asilimia 2.1 hadi
1.3.

"Bidhaa kwa ajili ya usafi wa nyumbani,mfano sabuni kutoka asilimia 4.6 hadi 3.0.Bidhaa na huduma za afya kutoka asilimia 2.5 hadi 1.8."

Pia,vifaa kwa ajili ya magari binafsi,mfano betri za magari kutoka asilimia 6.5 hadi 5.6, simu za mkononi kutoka asilimia 1.9 hadi 0.6.

Aida, kuna bidhaa na huduma kwa ajili ya starehe, michezo na utamaduni kutoka asilimia 3.3 hadi 3.0 na bidhaa na huduma kwa ajili ya usafi binafsi kutoka asilimia 7.2 hadi 5.9 .

Dkt.Chuwa amesema, mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwaka ulioishia mwezi Julai, 2024 umeongezeka kidogo hadi asilimia 1.0 kutoka asilimia 0.9 kwa mwaka ulioishia mwezi Juni, 2024.

Mfumuko wa Bei ambao haujumuishi bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwaka ulioishia mwezi Julai,2024 umepungua hadi asilimia 3.8 kutoka asilimia 4.0 kwa mwaka ulioishia mwezi Juni,2024.

Wakati huo huo,Mtakwimu Mkuu wa Serikali akielezea kuhusu hali ya mfumuko wa bei kwa baadhi ya nchi za Afrika Mashariki kwa mwaka ulioishia mwezi Julai,2024 amesema,

"Nchini Uganda, Mfumuko wa Bei kwa mwaka ulioishia mwezi Julai, 2024 umeongezeka hadi asilimia 4.0 kutoka asilimia 3.9 kwa mwaka ulioishia mwezi Juni, 2024."

Kwa upande wa Kenya,amesema Mfumuko wa Bei kwa mwaka ulioishia mwezi Julai, 2024 umepungua hadi asilimia 4.3 kutoka asilimia 4.6 kwa mwaka ulioishia mwezi Juni,2024.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news