DODOMA-Wanachama wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya ( NHIF) kwa sasa wanaweza kupata huduma za matibabu kwa kutumia namba ya kitambulisho cha Taifa kinachotolewa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA).
Hayo yamebainishwa leo na Kaimu Meneja Uhusiano wa NHIF, Grace Michael katika Maonesho ya Nanenane Kitaifa yanayoendelea mkoani Dodoma.
Kaimu Meneja huyo amesema, mfuko huo umeendelea kurahisisha huduma zake hususani ya utambuzi wa mwanachama anapokuwa katika vituo vya kutolea huduma kwa kutumia namba ya NIDA.
“Kwa sasa mwanachama wa NHIF anaweza akatambuliwa kituoni kwa kutumia namba ya NIDA. Hii itaondoa changamoto kwa wale waliokuwa wanasahau vitambulisho nyumbani.Mwanachama hatalazimika kutembea na kadi hata wale wanaopoteza hizo kadi nao wanaenda kuondoa usumbufu.
“Wanachama watumie fursa hii kuhuhisha taarifa zao za NIDA. Walioko hapa watenbelee banda letu,” amesema.
Pia, Grace Michael ametoa wito kwa wananchi kutumia fursa ya kujiunga na mfuko huo kwa sababu ugonjwa unampata mtu bila taarifa.