MOROGORO-Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), kupitia Ofisi ya Mkoa wa Morogoro, imeanza kampeni ya uhamasishaji na utoaji elimu kwa wananchi ili wajiunge na huduma za Mfuko huo ili kupata matibabu bila kikwazo cha fedha.
Kampeni hiyo imelenga kuwafikia wananchi katika maeneo yao kupitia nyumba za ibada, sokoni na maeneo yenye mikusanyiko ya wananchi.
Akizungumzia kampeni hiyo, Meneja wa NHIF Mkoa wa Morogoro,Bw. Mbala Shitindi amesema kuwa tayari wametembelea Kanisa Katoliki Parokia ya Ifakara, Kanisa la Kilutheri Tanzania Dayosisi ya Ulanga, Kanisa la Nayoth Devine Ministry na Mgodi wa Ruby ulioko Ifakara.
"Tumeamua kuja huku ili kukutana na wananchi katika ngazi ya kijiji, lengo kubwa wapate elimu na wajiunge na Mfuko ili wawe na uhakika wa kupata huduma za matibabu wakati wote, tutawafikia majumbani, magengeni na maeneo yote wanayopatikana," amesema Bw. Shitindi.
Aidha, kampeni hiyo ambayo imeanza leo na itahitimishwa Agosti 31, 2024, itaambatana na upimaji wa afya bure na utoaji wa elimu ya kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza.
Ametoa rai kwa wananchi wa maeneo hayo kutumia fursa hiyo kujiunga na NHIF na kupima afya bure.