DAR-Timu ya maafisa waandamizi kutoka Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) wamekuwa kivutio kikubwa kwa wananchi na mashabiki wa klabu za Simba na Yanga, kwa kutumia utaalamu wao kufikisha elimu ya bima ya afya kwa mmoja baada ya mwingine.
Ni kupitia mtanange wa Kariakoo Derby ambao ulikuwa nusu fainali ya Ngao ya Jamii iliyowakutanisha watani hao wa jadi Agosti 8,2024 katika Dimba la Benjamin Mkapa lililopo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar Es Salaam.
Kupitia mtanange huo ambao ulienda sambamba na maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wakulima (Nanenane),maafisa hao wa NHIF walitoa elimu na kufanya uhamasishaji mkubwa kwenye mtanange huo.
Mashabiki mbalimbali kutoka sehemu mbalimbali za nchi waliweza kupata nafasi ya Kuufahamu Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, majukumu yake, lakini aina mbalimbali ya huduma ambazo zinatolewa na mfuko huo.
Aidha,kwa nyakati tofauti tofauti mashabiki wameonesha kufurahishwa na tukio hili na wamekiri kuwa hii ni mara ya kwanza kwao kupata elimu kwenye tukio jubwa kama hili na wamewapongeza watumishi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kwa kufanya ubunifu huo.
Mashabiki wote ambao waliwahi uwanjani kuanzia najira ya saa 3 asubuhi waliweza kupata nafasi ya kuelimishwa na maafisa kutoka Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya.
Elimu hiyo iliendelea mpaka ndani ya uwanja huku ikiwapa fursa pana zaidi mashabiki kujifunza na kuuliza maswali mbalimbali kuhusu Bima ya Afya na kupata uelewa zaidi.
Kaimu Meneja wa Masoko na Huduma kwa Wateja ,Bi. Flora Mataba sanjari na Kaimu Meneja wa Ofisi ya NHIF Temeke, Cannon Luvinga kwa pamoja wamewahakikishia wananchi kuwa mfuko utaendelea na jitihada za kuelimisha wananchi kwenye kila mikusanyiko ili kuhakikisha wananchi wanapata nafasi ya kujiunga na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya bila changamoto yoyote.
Aidha, kampeni hii ya uhamasishaji ina lengo la kuwaandaa wananchi kwa Bima ya Afya kwa wote baada ya Sheria husika kupitishwa. NHIF inawezesha lengo la Serikali ya kuhakikisha kila mwananchi anapata Bima ya Afya.