ZANZIBAR-Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Mhe.Riziki Pembe Juma amesema jukumu la kumlinda mtoto juu ya matukio mbalimbali ya ukatili sio la Serikali pekee bali ni la kila mtu.
Mhe. Riziki ameyasema hayo wakati akitoa salamu kutoka Zanzibar, wakati wa ziara ya Kamati Tendaji ya Mradi wa "Hapana Marefu Yasiyo na Mwisho", huko Mkoa wa Mwanza.
Mhe. Riziki amesema kuwa Serikali zetu zote mbili zimekuwa zikishirikiana na wadau mbali mbali katika kuhakikisha maslahi ya jamii yanapatikana pamoja na kukemea na kupiga vita vitendo hivyo.
Amesema,Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inasimamia Sheria ya Mtoto nambari 6 ya Mwaka 2011 ambapo inamtambua mtoto ni kuanzia umri 0 hadi miaka 18, na hivo kupiga vita suala zima la ndoa kwa watoto wa umri huo na yeyote anayebainika kwenda kinyume na hilo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Hivyo amewaomba viongozi wa dini, Watendaji wa Serikali, Taasisi zisizo za Kiserikali NGI'S na wadau wote wa mradi huo kuhakikisha kila mmoja kwa nafasi yake kuwa na jukumu la kupiga vita ndoa za utotoni, kuziangalia Sheria zilizopo ili ziendane na azma nzima ya kutokomeza suala hilo.
Mhe. Riziki amesema Serikali ipo pamoja nao na ameuomba uongozi wa Kanisa la KKKT kwa kushirikiana na Serikali na wadau wengine kuangalia uwezekano wa kuwatatulia changamoto zao.
Mapema, Mwenyekiti wa Kamati ya Utendaji ya Mradi huo na Mkuu wa Kanisa Mstaafu wa KKKT, Dkt.Fredrick Onael Shoo, amesema ni vyema kuchukua hatua kwa pamoja na kuleta mabadiliko chanya juu ya suala zima la ndoa za utotoni ili kuwaacha huru watoto wa kike katika masomo yao.
Kwa upande wake Kiongozi Mkuu wa Mradi wa "Hapana Marefu Yasiyo na Mwisho,"mama Patricia Mwaikenda amesema lengo la mradi huo ni kuwashirikisha zaidi viongozi wa dini mbalimbali katika kuona wanasaidia na kuielimisha jamii na kukemea ndoa za utotoni.
Mradi huo unasimamiwa na Kanisa la KKKT, ukiwa na kauli mbiu "Ndoa za utotoni sasa mwisho".