DODOMA- Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Bi. Jenifa Christian Omolo, amefungua Kikao kazi cha mafunzo ya Mfumo wa Uandaaji na Usimamizi wa Bajeti (CBMS) ulioboreshwa ambacho kitaambatana na kufanya tathmini ya utekelezaji wa Bajeti ya Serikali ya Mwaka 2023/2024 ili kuweka mikakati itakayosaidia kuboresha uandaaji wa mipango na bajeti kwa mwaka 2025/2026.
Akizungumza jijini Dodoma kwa niaba ya Katibu Mkuu Dkt. Natu El-maamry Mwamba, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Bi. Jenifa Christian Omolo, alisema kuwa lengo la kikao hicho ni kupata mafunzo ya Mfumo wa CBMS ulioboreshwa na kujadili kuhusu mafanikio na changamoto zilizojitokeza wakati wa utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2023/2024 ili kubaini maeneo ya kuboresha.
Alisema kuwa,kikao kazi hicho kimegawanywa katika makundi mawili ambapo kundi la kwanza limeanza mafunzo na kundi la pili linatarajiwa kuanza mafunzo Agosti 21, 2024.
Bi. Omolo alisema kuwa ushiriki wa wajumbe katika Kikao kazi hicho utasaidia kuboresha utekelezaji na usimamizi wa bajeti ya Serikali, kuongeza ufanisi katika mchakato wa bajeti na kuhakikisha vipaumbele vya Serikali vinatekelezwa ipasavyo.
Vilevile aliwataka washiriki wa kikao kazi hicho kushiriki kikamilifu katika mafunzo na kuuliza maswali yatakayowezesha kuuelewa vizuri na kuutumia Mfumo huo wa CBMS ili kuimarisha utekelezaji na usimamizi wa bajeti ya Serikali.
Aidha, aliwafahamisha washiriki wa mafunzo kuwa mchakato wa maandalizi ya Mwongozo wa Mpango na Bajeti ya Mwaka 2025/2026 umeanza, hivyo ushauri na mapendekezo yatakayotokana na kikao kazi hicho yatasaidia katika kuboresha maandalizi ya Mwongozo huo.