KILIMANJARO-Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kimeunganisha wadau mbalimbali kujadili na kupata njia nzuri itakayofanikisha uwekaji wa darubini katika tambarare ya mlima Kilimanjaro ili kuchochea utalii wa anga kwa watalii wanaotembelea mlima huo.

Akiongea katika mkutano huo Mtaalam wa Astronomia na Mtafiti mkuu wa mradi huo, Dkt. Noorali Jiwaji, amesema majadililiano yamejikita katika kuhakikisha kuwa uwekaji wa darubini hiyo ambayo itasimikwa katika tambarare ya mlima Kilimanjaro baina ya vilele vya Kibo na Mawenzi haiwezi kuharibu mandhari ya mlima huo pamoja na shuguli za kiutalii zaidi iongeze watalii katika mlima huo.
Amesema, pia mkutano huu umekuwa ni mwendelezo wa mkutano wa awali uliofanyika katika mji wa Marangu mkoani Kilimanjaro ambao ulihusisha zaidi wenyeji kuzunguka hifadhi ya mlima Kilimanjaro wakiwemo watu binafsi, wafanyabiashara, mashule, vyuo na taasisi zinazosimamia shughuli za uhifadhi na utalii wa mlima huo ikiwamo mamlaka ya Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro (KINAPA).
Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kimekuwa na mkakati wa muda mrefu wa uwekaji wa darubini katika mlima Kilimanjaro ambapo watalii wataweza kushuhudia zao jipya la utalii wa anga kwa kuweza kutazama nyota na vivutio vipatikanavyo angani.
