NA DIRAMAKINI
BUNGE la Thailand limemchagua binti wa bilionea na kiongozi wa zamani wa nchi hiyo, Thaksin Shinawatra, Paetongtarn Shinawatra kuwa Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu mpya wa Thailand,Paetongtarn Shinawatra.(Picha na Mtandao).
Paetongtarn mwenye umri wa miaka 37 anakuwa Waziri Mkuu mwenye umri mdogo zaidi nchini Thailand na mwanamke wa pili kuwahi kushika wadhifa huo baada ya ndugu yake Yingluck.
Agosti 16,2024 wabunge wamemuidhinisha Paetongtarn kutoka chama cha Pheu Thai kuwa Waziri Mkuu kwa kupata kura 319 za ndio dhidi ya 145 za hapana.
Chama chake na washirika wake wanashikilia viti 314 kati ya 493 bungeni, na alihitaji kura angalau nusu ya wabunge wa sasa kuwa waziri mkuu.
Kuchaguliwa kwake kulitokea siku mbili baada ya Srettha Thavisin aliyekuwa akishikilia wadhifa huo kuondolewa na Mahakama ya Kikatiba nchini humo.
Waziri Mkuu huyo mpya anakabiliwa na kibarua kigumu cha kufufua uchumi wa Thailand na kuepuka mapinduzi ya kijeshi na uingiliaji kati wa mahakama ambao umeondoa tawala nne zilizopita nchini humo.
Paetongtarn ni mtu wa tatu kutoka katika familia yake kuchukua majukumu makubwa nchini humo.
Baba yake, Thaksin alikua waziri mkuu kupitia chama cha Thai Rak Thai Party mwaka 2001 hadi alipoondolewa madarakani kupitia mapinduzi ya kijeshi mwaka 2006.
Dada yake Thaksin, Yingluck Shinawatra ambaye ni shangazi yake Paetongtarn alikua waziri mkuu mwaka 2011 hadi alipoondolewa na Mahakama ya Kikatiba mwaka 2014 baada ya kumfukuza Thawil Pliensri kutoka Baraza la Usalama la Taifa mwaka 2011.
Tukio hilo lilifuatiwa na mapinduzi mengine ya kijeshi mwaka 2014, kufuatia miezi kadhaa ya misukosuko ya kisiasa nchini Thailand. Thaksin na Yingluck waliondoka Thailand ili kuepuka kukamatwa hadi Thaksin aliporudi Thailand Agosti 2023.
Pamoja na kuwa mtu mdogo zaidi kuchukua uongozi, Paetongtarn ndiye waziri mkuu wa pili wa kike wa Thailand baada ya shangazi yake.