NA DIRAMAKINI
DIMBA la 30 June Air Defence Stadium jijini Cairo limegeuka karaa kwa wawaklishi wa Tanzania, JKU FC baada ya kupokea kichapo cha mabao 6-0 kutoka kwa Pyramids FC ya nchini Misri.
Ni katika mchezo wa hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika uliochezwa Agosti 18,2024 jijini Cairo.
Fiston Mayele ndiye aliyeanza na bao la kwanza dakika ya 8' ya kipindi cha kwanza huku dakika ya 14 Walid El Karti akitupia lingine.
Kabla bao hilo halijapoa, Mohanad Lasheen dakika ya 26 alitupia bao la tatu huku Ibrahim Adel dakika ya 31 akiongeza la nne.
Hadi kipindi cha kwanza kinafikia tamati,JKU FC walikuwa hoi kwa mabao manne kutoka kwa Pyramids FC jambo ambalo liliwapunguza kasi ya kusaka ushindi.
Aidha, kipindi cha pili kilianza kwa Pyramids FC kutembeza kichapo tena ambapo dakika ya 51,Mohanad Lasheen alitupia bao la tano na dakika ya 88,Mahmoud Mohamed alifunga hesabu ya nusu dazeni ya mabao hayo.
Matokeo hayo, yameiweka njia panda JKU FC kwani katika mchezo wa marudiano wakikosa ushindi wa mabao saba watakuwa hawana lao tena.