Rada zaipaisha Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) Kimataifa

NA GODFREY NNKO 

MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imeishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uwekezaji mkubwa wa miundombinu ya hali ya hewa nchini, hatua ambayo imewezesha Tanzania kuendelea kuheshimika duniani huku ikipewa kipaumbele katika masuala yanayohusu hali ya hewani.
Shukurani hizo zimetolewa leo Agosti 24,2024 na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa,Dkt.Ladislaus Chang’a.

Dkt.Chang’a alikuwa anazungumzia kuhusu mafunzo ya matumizi ya Data na Taarifa za Rada za Hali ya Hewa ambayo yatatolewa na Chuo cha Taifa cha Hali ya Hewa kinachoendeshwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA).

Ni kwa kushirikiana na Kitengo cha Elimu na Mafunzo cha Shirika la Hali ya Hewa Dunia jijini Mwanza.

"Nichukue fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu, na pia Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ajili ya kazi kubwa ambayo inaendelea kufanyika ya kuimarisha miundombinu na huduma za hali ya hewa hapa nchini.

"Ni kutokana na huo uwekezaji ambao umefanyika kwa ukubwa,Tanzania kupitia Mamlaka ya Hali ya Hewa tumepata fursa, tumepewa kibali cha kuweza kuandaa mafunzo ya rada za hali ya hewa kwa nchi za Afrika Mashariki na Nchi za Kusini mwa Afrika."

Amesema, mafunzo hayo yanatarajiwa kufanyika kuanzia Agosti 26 hadi Agosti 30,2024 jijini Mwanza.

"Mafunzo hayo yatajumuisha nchi takribani 12 kutoka Ukanda wa Afrika Mashariki, lakini pia Kusini mwa Afrika.

"Nchi 12,zitaleta wawakilishi wawili wawili katika kushiriki mafunzo ya Rada, mafunzo hayo yatafanyika hapa Tanzania kutokana na uwekezaji mkubwa ambao umefanywa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika miundombinu ya Rada za hali ya hewa."

Dkt.Chang’a amesema, hivi karibuni mamlaka hiyo imekamilisha kufunga Rada ya Hali ya Hewa mkoani Mbeya.

"Lakini, pia na Rada ya Hali ya Hewa kule Kigoma,na tunatarajia zitaanza kufanya kazi vizuri kwa ajili ya utoaji wa huduma za hali ya hewa hususani katika kutoa tahadhari ya hali mbaya ya hewa."

Amesema, mafunzo hayo ni maalum kwa wataalam ambao wanafanya kazi za hali ya hewa katika nchi zao ili waweze kujengewa uelewa,weledi na umahiri katika kutumia Rada za hali ya hewa.

Washiriki wa mafunzo hayo ni wataalamu kutoka Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Burundi, Comoro, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Kenya, Msumbiji, Malawi, Mauritius, Rwanda, Seychelles, Sudan Kusini, Zambia na Uganda.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news