ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema kuwa, wakati umefika kwa Mali na Tanzania kuimarisha uhusiano ambao umezorota baina ya nchi hizo.
Dkt. Mwinyi ameyasema hayo Agosti 14, 2024, alipokutana na Balozi mpya wa Mali, Mhe. Madou Diallo, aliyefika Ikulu kujitambulisha rasmi.
Aidha, amefahamisha kuwa kwa vile historia za Mji wa Timbuktu, Mali na Mji Mkongwe, Zanzibar ni miji ya urithi, ni vema kukawa na ushirikiano maalum katika eneo hilo.
Dkt. Mwinyi amesema ni vema kwa sasa nchi hizo mbili kuanzisha ushirikiano wa kibiashara utakaotoa manufaa kwa wafanyabiashara wa pande zote mbili.
Kwa upande wake, Balozi Madou Diallo amemuelezea Rais Dkt. Mwinyi kuwa uhusiano wa nchi za Afrika ni muhimu ili kuendeleza fikra za viongozi waliopigania uhuru wa nchi hizo. Balozi Diallo ameongeza kuwa, kuna maeneo mengi ya ushirikiano wa kiuchumi yanayoweza kuanzishwa baina ya Mali na Tanzania hasa wakati huu ambapo amani imeimarika nchini Mali.