ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema, China imekuwa ikiisaidia Zanzibar katika mambo mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya hospitali.

Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi ameyasema hayo Agosti 26, 2024, Ikulu Zanzibar, alipozungumza na timu ya madaktari 29 kutoka kundi la 33, walioongozwa na Kaimu Balozi Mdogo wa China Zanzibar, Chang Ming, chini ya kiongozi wa madaktari hao, Dk. Yuzheng Huang, waliofika kumuaga baada ya kufanya kazi nchini kwa kipindi cha mwaka mmoja.
Aidha, Dkt. Mwinyi ameishukuru Serikali ya China kwa ushirikiano wake na Zanzibar kupitia sekta mbalimbali za maendeleo, ikiwemo sekta ya afya, unaochangiwa na uhusiano wa kidiplomasia uliopo baina Zanzibar na China tangu kuasisiwa kwake.
Halikadhalika, Dk. Mwinyi amesema kuwa mbali na misaada hiyo, China pia imeisaidia Zanzibar kwa kutoa msaada wa kitaalamu katika udhibiti na kinga za maradhi mbalimbali, ikiwemo kichocho kwa Unguja na Pemba, pamoja na kuleta teknolojia mpya ya uchunguzi wa maradhi ya kansa.