Rais Dkt.Mwinyi aitaka ATCL kuongeza safari za Kimataifa kupitia Zanzibar

ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amelishauri Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kuongeza safari za kimataifa kupitia Zanzibar kwa lengo la kukuza utalii pamoja na kufungua kisiwa cha Pemba kiutalii kutokana na vivutio lukuki ambavyo vinahitaji kutangazwa.
Rais Dk. Mwinyi ameyasema hayo alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, wakati wa Uzinduzi na Mapokezi ya ndege mpya ya Boeing 787-8 Dreamliner, iliyowasili nchini Agosti 20,2024 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume.

Ndege hiyo mpya, ambayo ni ya 16 kununuliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imetoka moja kwa moja Marekani, imeigharimu shilingi bilioni 300.

Halikadhalika, Dk. Mwinyi amesema Serikali itaendelea kuwekeza katika sekta ya anga kwani ni njia muhimu ya kufungua milango ya kiuchumi na kuunganisha nchi na mataifa mengine kimaendeleo.
Aidha, amebainisha kuwa kuimarisha Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2020-2025.

Kwa upande mwingine, Dk. Mwinyi amezipongeza juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan za kuendeleza na kuimarisha Shirika la Ndege la Tanzania, kwani limeijengea heshima kubwa nchi na kuwa miongoni mwa mashirika yenye ndege nyingi kwa nchi za Kusini mwa Afrika.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news