ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amewaongoza viongozi na wananchi katika mazishi ya marehemu Hassan Omar (Mkele), aliyefariki jana.
Marehemu Hassan Omar Mkele alikuwa miongoni mwa Watanzania wanne walioshiriki kuchanganya udongo wa Muungano takriban miaka 60 iliyopita, wakati Tanganyika na Zanzibar zikiungana.
Mapema, Alhaj Dk. Mwinyi alijumuika na waumini wa dini ya Kiislamu katika sala ya maiti katika Msikiti wa Kibweni Mshelishelini, Wilaya ya Magharibi A, Mkoa wa Mjini Magharibi.Baada ya maziko, Alhaj Dkt. Mwinyi alifika nyumbani kwa marehemu kuwafariji na kuwapa pole wafiwa, na kuwataka kuwa na subira wakati huu wa msiba mzito.