ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi amewaongoza wananchi na viongozi mbalimbali katika maziko ya mwanasiasa mkongwe, marehemu Mvita Mussa Kibendera, aliyefariki Agosti 26,2024.
Mapema, Alhaj Dk. Mwinyi alijumuika na waumini wa dini ya Kiislamu katika sala ya maiti iliyofanyika Msikiti wa Mwembeshauri, wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Marehemu Mvita Kibendera wakati wa uhai wake aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali katika Chama Cha Mapinduzi na Serikali, ikiwemo Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, Katibu wa CCM Wilaya ya Mjini, na Mwenyekiti wa CCM jimbo la Kikwajuni.
Baada ya maziko, Alhaj Dkt. Mwinyi alifika nyumbani kwa marehemu Maungani kuwafariji na kuwapa pole wafiwa, na kuwataka kuwa na subira katika kipindi hiki cha msiba mzito.Viongozi mbalimbali walijumuika katika maziko hayo akiwemo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla, na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Othman Masoud Othman.