ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt.Hussein Ali Mwinyi amesema, kuna haja kwa Serikali kuangalia kwa karibu miundombinu duni ya madrasa, maslahi ya walimu wa madrasa na maimamu wa misikiti.
Alhaj Dkt.Mwinyi ameyasema hayo leo Agosti 23, 2024 Ikulu jijini Zanzibar alipokuwa akizungumza na wajumbe wa Baraza la Ulamaa Zanzibar waliofika kumtembelea.
Amesema kuwa, miundombinu ya madrasa, maslahi ya walimu wa madrasa na maimamu wa misikiti nchini ni dhaifu mno.
Vile vile ameongeza kuwa, ni vema Serikali kwa kushirikiana na vyombo vya kidini kuangalia njia bora ya kufanya kazi na kusaidia kutatua changamoto hizo.
Alhaj Dkt.Mwinyi amelisihi baraza hilo kuendelea kuisimamia amani na utulivu kwa kutumia lugha moja kupitia viongozi wao, maimamu wa misikiti, pamoja na wanasiasa kwenye majukwaa yao ili kuendeleza taifa lenye umoja na mshikamano.
Naye Mufti Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Saleh Omar Kaabi amepongeza juhudi za maendeleo anazozisimamia Rais Dkt.Mwinyi hasa kwa kipindi kifupi cha uongozi wake.
Pia, amemuahidi Alhaj Dkt. Mwinyi ushirikiano wa hali ya juu kutoka kwa baraza hilo kupitia misingi ya Qur'an, Hadithi, Fiqhi na Tafsiri, pamoja na kufuata miongozo na Sunnah za Mtume (S.A.W) hasa katika suala la kusimamia ustawi, amani na utulivu wa nchi.