ZANZIBAR-Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amewahakikishia wananchi kuwa Serikali inaendelea na ujenzi wa barabara mijini na vijijini, na imepanga hivi karibuni kujenga barabara ya kisasa kuanzia Tunguu hadi Makunduchi yenye urefu wa kilomita 43.Amesema barabara hiyo itakuwa na njia nne, taa, njia za wapita kwa miguu, mitaro ya maji, pamoja na bustani.
Dk. Mwinyi ameyasema hayo leo Agosti 13,2024, ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya kuzungumza na Wajumbe wa Kamati za Siasa za Halmashauri Kuu ya CCM za Tawi, Wadi, Jimbo, Wilaya, na Mkoa wa Magharibi kichama katika Ukumbi wa Mikutano, Viwanja vya Maonesho Nyamanzi, Dimani.
Aidha, Dk. Mwinyi amesema kuwa uwepo wa vyama vingi ni kukuza demokrasia na siyo kuleta chuki na ubaguzi nchini, na amewataka wanasiasa kuhubiri amani na kunadi sera za maendeleo kwa wananchi.
Vilevile, Dk. Mwinyi amewahimiza wanachama wa CCM kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ili kuwa na sifa ya kushiriki Uchaguzi Mkuu mwakani na kukihakikishia Chama Cha Mapinduzi ushindi wa kishindo.
Kwa upande mwingine, Dk. Mwinyi amewasisitiza viongozi wa CCM ngazi zote kunadi mafanikio ya Ilani ya Utekelezaji ya CCM 2020-2025 katika sekta mbalimbali zilizotekelezwa na Serikali kwa asilimia mia moja.