Rais Dkt.Samia atoa maagizo kwa mawaziri wote kuhusu fedha za umma

NA GODFREY NNKO

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan amewataka mawaziri wote kuhakikisha fedha zinazoingizwa kwenye sekta zao zinakwenda kutatua kero za wananchi.
Mheshimiwa Rais Dkt.Samia ameyasema hayo leo Agosti 1,2024 wakati akiwasalimia wananchi eneo la Pugu Stesheni jijini Dar es Salaam.

Ni muda mfupi baada ya kuzindua rasmi miundombinu ya huduma za usafiri wa reli ya kimkakati ya SGR na treni ya umeme inayofanya safari zake kutoka Dar es Salaam,Morogoro hadi Dodoma.

SGR ni moja ya miradi ya kimkakati inayoendelezwa chini ya uongozi wa Rais wa Awamu ya Sita,Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.

"Ninazindua safari ya kwanza ya treni kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma,kazi kubwa imefanyika.Lakini, si hiyo tu tunaendelea kujenga reli mpaka tufike Kigoma tuungane na nchi jirani ili tuweze kufanya biashara zetu vizuri.

"Lakini, kwa kuwa stesheni kubwa ya reli hii ipo hapa Pugu nikawaambia lazima nisimame niwasalimie wanangu.
Hata hivyo, Mheshimiwa Rais Dkt.Samia amewahidi wakazi wa Pugu kuja kuwaeleza mengi zaidi akifanya ziara Mkoa wa Dar es Salaam.

"Kwa hiyo nikija tutazunguza zaidi. Ninataka niwaahidi kwamba pesa yote inayokusanywa na hapa nimpongeze sana Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Jiji.

"Pesa yote inayokusanywa siyo hapa Pugu tu, lakini Tanzania nzima inayoingia kwenye akaunti za Serikali kwenye Hazina ya Serikali, hiyo pesa ni ya wananchi.

"Mimi sioni sababu ya kukaa nayo kule na wananchi wakawa na shida huku, kwa hiyo ni maagizo yangu kwa Waziri wa Fedha na Mawaziri wote, fedha zinazoingizwa kwenye sekta zao zikafanye kazi ya kuondosha kero za wananchi.

"Hiyo ndiyo ahadi yangu wananchi na tutaendelea kufanya hivyo, tutaondosha kero ya elimu, kero ya afya, kero ya maji na kero zote zinazowakabili wananchi.

"Lakini, kama mnavyojua maendeleo ni safari, tunakwenda hatua moja kwenda nyingine...kwenda nyingine.
"Lakini, ninadhani ninyi ni mashahidi katika kipindi hiki cha miaka mitatu, safari hii ya maendeleo tumekwenda nayo haraka sana.Kwa hiyo, tunaposema Kazi Iendelee maana yake Kazi Iendelee,"amesisitiza Mheshimiwa Rais Dkt.Samia kabla ya kuanza safari kuelekea Morogoro kwa treni ya SGR.

Wakati huo huo, Mheshimiwa Rais Dkt.Samia amewahidi wananchi wa Morogoro kuwa,Serikali inakwenda kutatua changamoto ya miundombinu ya barabara.

Rais Dkt.Samia ameyabainisha akizindua rasmi Mradi wa Mkakati wa Treni ya Umeme ya SGR Dar es Salaam hadi Dodoma katika Kituo cha Ngerengere mkoani Morogoro.

Reli ya SGR kutoka Dar es Salaam kupitia Morogoro hadi Dodoma ina urefu wa kilomita 722, ikiwa ni sehemu ya awamu ya kwanza ya ujenzi wa mradi wa SGR kuelekea mikoa ya Magharibi na Kanda ya Ziwa.

Safari ya kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro hutumia saa moja na dakika 45 huku kutokea Dar es Salaam hadi Dodoma ikitumia saa tatu na dakika 25, huku ikiwa na uwezo wa kubeba tani 10 za mizigo.

"Nimesikiliza vizuri wabunge wenu (Morogoro) walichosema, hawana shida ya elimu wala afya wala maji. Kazi inaendelea si ndiyo? Umeme kazi inaendelea.

"Shida waliyonieleza ni shida ya barabara si ndiyo na walisema tayari mkataba ulishasainiwa...na Mkandarasi ameshapatikana. Niwahakikishie barabara itajengwa. Itajengwa kwa sababu hiyo barabara inayosemwa na mimi pia ninaitumia barabara hiyo.

"Nilikuwa nina mashamba makubwa pale Mvuha basi mkanitilia ng'ombe wakala mpunga wangu nikakimbia.

"Lakini, nina mashamba pale Msonge ambayo pia ninataka kuyaendeleza sasa na barabara ni hiyo hiyo,kwa hiyo niwahakikishie barabara itajengwa.

"Kwa sababu mimi nami ni mwana Morogoro pia,kwa hiyo niwapongeze kwa reli mpya ambayo inapita, lakini niwapongeze kwa mema yote ambayo yamefanyika,"amesisitiza Rais Dkt.Samia.

Aidha,Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kufanya ziara ya siku sita mkoani Morogoro ndani ya mwezi huu.

Akitoa taarifa ya ziara ya Rais Dkt.Samia, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima alisema ziara hiyo itaanza Agosti 2 hadi 7, mwaka huu.

Kwa mujibu wa mkuu wa mkoa huyo, katika ziara hiyo, Rais Samia anatarajiwa kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo ndani ya mkoa ikiwemo ya ujenzi vituo vya afya,kilimo na viwanda.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news