Rais Dkt.Samia awaalika wawekezaji Kilombero,Malinyi na Ulanga

MOROGORO-Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amewahakikishia wawekezaji uwepo wa umeme wa uhakika katika Wilaya za Kilombero, Malinyi na Ulanga na hivyo amewaalika kwenda kuwekeza katika maeneo hayo.Rais, Dkt. Samia ameyasema hayo Agosti 05, 2024 wakati akihitimisha ziara yake katika Mji wa Ifakara Wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro ambapo amesisitiza kuwa uongezaji thamani wa bidhaa katika viwanda unahitaji uwepo wa umeme wa uhakika hivyo Serikali inafanya kila jitihada ili nchi iweze kujitosheleza na nishati hiyo na kuwezesha uongezaji thamani malighafi zinazopatikana nchini ikiwemo mazao.
Amewahakikishia wawekezaji kuwa, maeneo ya Kilombero, Malinyi na Ulanga yatakuwa na umeme wa kutosha hivyo wawekezaji wasisite kuendelea kuwekeza katika viwanda mbalimbali.
Ameongeza kuwa, kupatikana kwa umeme katika maeneo hayo kumeendelea kuwavutia wawekezaji wa ndani ambao wameweka mashine za kuchakata nafaka na kuongeza kuwa ujenzi mkubwa wa maghala unaendelea.

"Uwekezaji huu unaonesha kwamba umeme umeleta faida kubwa ndani ya maeneo haya, niwahakikishie Serikali itaendelea kusimamia Sekta ya Nishati ili kuendelea kuwa na umeme wa uhakika,"amesisitiza Dkt.Samia.
Akizungumzia miradi ya umeme vijijini, amesema Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imeshapeleka umeme kwenye vijiji vyote 110 vya Wilaya ya Kilombero.

Ameongeza kuwa, kazi inayoendelea sasa ni upelekaji wa umeme kwenye Vitongoji na kwenye Taasisi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news