Rais Dkt.Samia kushiriki uapisho wa Rais mteule Paul Kagame

NA GODFREY NNKO

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajia kusafiri kuelekea Jamhuri ya Rwanda kesho asubuhi kushiriki sherehe za uapisho wa Rais mteule, Mhe. Paul Kagame ambaye alichaguliwa kuwa Rais wa nchi hiyo mwezi Julai,2024.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan akiwa na mgeni wake Rais wa Rwanda, Mhe. Paul Kagame mara baada ya mazungumzo yao Ikulu jijini Dar es Salaam yaliyofanyika Aprili 27, 2023. Rais wa Rwanda Kagame aliwasili nchini kwa ajili ya ziara ya kikazi ya siku mbili.(Picha na Maktaba).

Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Agosti 10,2024 na Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu,Sharifa B. Nyanga.

Rais mteule Paul Kagame anatarajiwa kuapishwa kesho Agosti 11, 2024.

Akitangaza matokeo ya uchaguzi huo mwezi uliopita Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi,Oda Gasinzigwa alisema,Mheshimiwa Paul Kagame alipata kura zaidi ya milioni 8.8, ambazo ni sawa na asilimia 99.18 ya kura zote halali zilizopigwa na kuhesabiwa.

Baada ya kutangazwa matokeo hayo, Mheshimiwa Paul Kagame aliwapongeza wananchi wote walioshiriki zoezi la uchaguzi ikiwemo kuendelea kuonesha imani kwake.

"Ushindi wa matokeo haya mnaouona ni muungano wa wafuasi wa wanachama wetu wa RPF kwa ushirikiano na wafuasi wa vyama vingine washirika wetu.’’

Frank Habineza kutoka Green Party of Rwanda baada ya kutolewa matokeo alimpongeza Rais Paul Kagame kwa ushindi huo.

Naye Pillipe Mpayimana mgombea binafsi alisema, hata kama hesabu zinaonesha ameshindwa, lakini bado ana imani kwamba atafanya vizuri siku za usoni.

Katika uchaguzi huo, zaidi ya watu milioni tisa walijiandikisha katika daftari la wapiga kura huku milioni mbili kati ya hao wakipiga kura.

Hiyo ilikuwa ni kwa mara yao ya kwanza, wengi wao wakiwa ni vijana wa chini ya miaka 20.

Aprili mwaka 2000, Paul Kagame aliteuliwa kuwa Rais wa Rwanda katika mkutano wa pamoja wa Bunge na Baraza la Mawaziri.

Aidha, Agosti mwaka 2003, Paul Kagame alipata ushindi kwenye uchaguzi wa urais ulioshirikisha kwa mara ya kwanza vyama vingi vya siasa na uchaguzi wa mwaka 2017 alishinda tena.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news