REA itaendelea kufanya tafiti za Nishati Safi za Kupikia-Mhandisi Saidy

ZANZIBAR-Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Hassan Saidy amesema wakala utaendelea kufanya tafiti za bidhaa za Nishati Safi za Kupikia ili kubaini ufanisi wa teknolojia zinazosambazwa kwa wananchi.
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Hassan Saidy (katikati) akizungumza jambo alipotembelea Banda la Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) ambao ni wazalishaji wa Mkaa Mbadala maarufu kama Rafiki Coal Briquettes. Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Dkt. Venance Mwasse.

Mhandisi Saidy amesema hayo Agosti 23, 2024 alipotembelea Banda la Wakala katika Tamasha la Kizimkazi eneo la Kizimkazi Dimbani Mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar.

"Tutaendelea kufanya utafiti wa bidhaa mbalimbali za Nishati Safi za Kupikia ili kutimiza dhamira ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha Nishati Safi ya Kupikia kwa wote inapatikana kwa gharama nafuu na yenye ufanisi," amesema.

Amesema,dhamira ni kuwa na teknolojia sahihi, rafiki na yenye gharama nafuu ili kumuwezesha na kumrahisishia kila Mwananchi kuwa na bidhaa bora.

"Tutahakikisha lengo la Serikali kupitia Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia 2024-2034 la kufikisha asilimia 80 ya wananchi wanaotumia Nishati Safi ya Kupikia ifikapo 2034 linafikiwa," amesema.
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Hassan Saidy akizungumza na watumishi wa REA kwenye Banda la Maonesho la REA katika Tamasha la Kizimkazi linalofanyikia eneo la Kizimkazi Dimbani Mkoa wa Kusini Unguja.

Mhandisi Saidy vilevile alitembelea mabanda ya Wadau wanaojihusisha na uandaaji, uuzaji na usambazaji wa Nishati Safi ya Kupikia na kujadiliana masuala mbalimbali hususan namna bora ya kuendelea kuboresha bidhaa zao ili kuleta tija inayokusudiwa.

Awali kabla ya kutembelea Maonesho ya Kizimkazi, Mhandisi Saidy alishiriki Kongamano la Nishati Safi ya Kupikia lililoandaliwa na Taasisi ya Mwanamke Initiatives Foundation (MIF) na Benki ya Uwekezaji ya Tanzania (TIB) kwa kushirikiana na Wizara ya Nishati na Taasisi zake ikiwemo REA ambapo Wakala ulipata fursa ya kuelezea suala la Upatikanaji wa Fedha katika kuendeleza Nishati Safi ya Kupikia.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news