DODOMA-Wanafunzi kutoka Shule za Sekondari Itega na Lukundo wamevutiwa na Banda la Wakala wa Nishati Vijijini (REA) hususan teknolojia ya kisasa ya Nishati Safi ya Kupikia.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti Agosti 6, 2024 walipotembelea Banda la REA wanafunzi hao walisema wamehamasika kushuhudia mambo makubwa yanayofanywa na Serikali hususan katika kuhamasisha matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia pamoja na namna ambavyo Serikali imejizatiti kupeleka maendeleo maeneo ya vijijini.

"Tumejifunza kuhusu teknolojia ya kisasa na matumizi ya Nishati Safi ya kupikia ambayo imelenga kuboresha mazingira. Hii imetuongezea uelewa kwa yale tunayofundishwa shuleni," amesema Irene Robert, Mwanafunzi wa Kidato cha Kwanza Sekondari ya Itega.

Wanafunzi hao wamekiri kuondoka na elimu ambayo hawakuwa nayo hapo awali kabla ya kutembelea Banda la REA.