NJOMBE-Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umewaasa wananchi kutunza mazingira na kulinda miundombinu pamoja na vyanzo vya maji ili kuendelea kupata huduma ya umeme pamoja na kuwa na miradi endelevu ya kufua umeme. Mkurugenzi wa Teknolojia za Nishati Jadidifu na Mbadala kutoka REA, Mhandisi Advera Mwijage ametoa rai hiyo wilayani Ludewa Agosti 27, 2024 alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya matengenezo ya mitambo ya kufua umeme kwa kutumia maporomoko ya maji ya mradi wa Lugarawa.
Mradi wa Lugarawa unasimamiwa na Kampuni ya Madope na unamilikiwa kwa ushirikiano baina ya Kanisa Katoliki Jimbo la Njombe, Watumia Umeme Ludewa (wananchi) na Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa.
Mhandisi Advera alifafanua kuwa mradi unatumia Nishati Safi na Salama kutokana na maporomoko ya maji hivyo ili mradi uwe endelevu wananchi washirikiane kutunza mazingira.
Akizungumzia dhumuni la ziara yake katika mradi, Mhandisi Advera alisema mradi huo wa Madope ni miongoni mwa miradi ya kufua umeme kwa kutumia Nishati Jadidifu inayowezeshwa na REA.
"Nimefika hapa kukagua shughuli zinazoendelea za matengenezo ya mitambo, kama mnavyotambua REA inawezesha miradi hii; kuna fedha ya Serikali hapa; hivyo ni wajibu wetu kuhakikisha kila kitu kinakwenda vizuri na kuhakikisha uzalishaji unaendelea," alifafan
Alisema zaidi ya wateja 5,000 walikuwa wanahudumiwa na mradi lakini tangu umesimama kutokana na hitilafu iliyojitokeza wateja hao kwa sasa wanahudumiwa na TANESCO kupitia miundombinu ya usambazaji iliyojengwa na REA.
Alisema mara baada ya matengenezo kukamilika; umeme utakaozalishwa na mradi utaingizwa katika Gridi ya Taifa kupitia miundombinu iliyopo.
Kwa upande wake Meneja wa Mradi, Mhandisi Masanja Kurwa alisema mradi uliwezeshwa na REA na kwamba ulianza rasmi kuzalisha umeme tarehe 30 Agosti, 2019 ambapo ulikuwa ukihudumia Vijiji 20 katika Kata 6 Wilayani humo.
Alisema mradi ulisanifiwa kuzalisha Kilowat 1,700 lakini haukuweza kufikisha na hivyo Serikali ilielekeza kusimamisha uzalishaji ili kufanya maboresho ya mitambo ili kufikia lengo.
"Tunaishukuru sana REA kwa kuendelea kutushika mkono tangu hatua za awali kabisa za ujenzi na hata sasa katika haya maboresho tunayofanya tayari tumepewa fedha na REA na sasa tunasubiri Mkandarasi akamilishe ili tuuze umeme kwa TANESCO," alisema Mhandisi Kurwa.
Mhandisi Kurwa amesema wanamtarajia Mkandarasi ambaye ni Kampuni ya ZECO mwenye makao makuu yake Nchini Italia kufika hapo kwa ajili ya maboresho na kwamba taratibu zingine zimekamilika.
Tags
Habari
Mazingira
Miundombinu ya Nishati
REA Tanzania
Vyanzo vya Maji
Wakala wa Nishati Vijijini (REA)
Wizara ya Nishati Tanzania