Serikali ina matarajio makubwa kwa TASAF kuzikwamua kiuchumi kaya maskini-Rais Dkt.Mwinyi

ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameeleza matarajio yake kwa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) katika kupambana na umaskini nchini.
Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo Ikulu jijini Zanzibar alipozungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa wa Mfuko huo, Shedrack Salmin Mziray aliyefika kujitambulisha kufuatia uteuzi wake hivi karibuni.

Amesema, anatarajia kupitia miradi ya TASAF kwa kaya maskini nchini, itaendelea kuzisaidia kaya zilizo kwenye mazingira magumu zaidi kwa lengo la kuwatoa kwenye umasikini mkubwa sambamba na kutafuta mbinu mbadala kwa kaya zinazoendelea kuwa kwenye umasikini uliokithiri licha ya kupitiwa na miradi ya TASAF.

Rais Dkt.Mwinyi pia ameupongeza uongozi wa TASSAF kwa jitihada zao za kuinua ustawi wa jamii hasa kwa kuboresha maisha ya familia 22,000 za Zanzibar kupitia mwendelezo wa miradi 15 yenye thamani ya shilingi bilioni 3.1 vikiwemo vituo vya afya, madarasa, maji safi na salama pamoja na barabara za vijijini.

Pia Rais Dkt. Mwinyi amesema, miundombinu hiyo imesaidia kukuza uchumi wa wananchi, kuwaongezea kipato, kwa kuzisaidia kaya masikini kukuza mitaji yao ya biashara na kuwaongezea ajira ndogondogo. Vilevile Rais Dkt. Mwinyi amepongeza mpango wa TASAF awamu ya pili kwa kuendeleza na kusaidia maeneo ambayo serikali zote mbili bado hazijakamilisha.

Naye, Mkurugenzi Mziray amemueleza Rais Dkt. Mwinyi kwamba kwa sasa TASAF inatekeleza kipindi cha pili cha awamu ya tatu ya miradi yake tangu mwaka 2020 hadi kukamilika kwake mwezi Septemba mwaka 2025 ambapo TASAF inatekelezwa na Mamlaka za utekelezaji 187, zikiwemo Halmashauri zote za Tanzania Bara, Unguja na Pemba.

Amesema, TASAF inashughulika na asilimia 26 ya kaya masikini nchi nzima na asilimia nane ni kaya masikini zaidi ziliwemo kaya milioni 1.3 wanazozipatia ruzuku kila baada ya miezi miwili na ajira za muda kwa watu wenye uwezo wa kufanyakazi.

Mkurugenzi huyo ameongeza kuwa, wanazisaidia kaya hizo kuweka vikundi vya maendeleo kwa kuweka na kuwekeza ili kuwaongezea mitaji kwa wastani wa shiingi laki tatu na nusu ili wajiendeleze zaidi.

Ameeleza kwa sasa TASAF inazishughulikia kaya 394,000 ambazo mradi umezifanyia tathmini na zina mafanikio mkakubwa kati ya hizo kaya 22,000 kutoka Zanzibar ambapo kati yao kaya18,000 zimenufaika na ruzuku za ziada za laki tatu tatu, wanaofanikiwa wanatolewa kwenye mpango kupisha waliokua hawajafanikiwa.Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF),Bw. Shedrack Salmin Mziray aliteuliwa kushika wadhifa alionao sasa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan Julai 3, mwaka huu.

Kabla ya uteuzi wake, Bw. Mziray alikuwa Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Ndani wa TASAF, awali aliikaimu nafasi hiyo ya Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF tokea Julai 1,mwaka 2023 baada ya kustaafu kwa aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji Bw. Ladislaus Joseph Mwamanga hadi alipoteuliwa yeye mwezi mmoja uliopita.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news