MANYARA-Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) amesema, Serikali itatoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami wilayani Mbulu Mkoa wa Manyara.Ameyasema hayo leo Agosti 23,2024 wakati akiwa mgeni rasmi katika Jubilee ya kutimiza miaka 25 ya Upadre ya Mhashamu Askofu Antony Gasper Lagwen wa Jimbo Katoliki Mbulu iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Bikira Maria Mpalizwa Mbinguni Mjini Mbulu mkoani Manyara.
Mheshimiwa Waziri ameahidi kuwa,Serikali itatoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara yenye urefu wa kilometa 50 itakayojengwa kwa kiwango lami kutoka Hydom-Labay hadi Garbabi kuanzia robo ya kwanza ya mwaka huu wa fedha (2024/2025).
Barabara hiyo inatajiwa kugharimu shilingi bilioni 12 na itakapokamilika itarahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji wa abiria na mizigo kwa wakazi wa wilaya hiyo na Mkoa wa Manyara kwa ujumla.