Serikali kufanya tathimini ya wakimbizi kurejea kwa hiari nyumbani kwao ifikapo Januari 2025

KIGOMA-Serikali imesema katika kuhakikisha kuwa Wakimbizi wa Burundi wanaohifadhiwa hapa nchini wanapata suluhisho la kudumu ifikapo Januari 2025 itafanya zoezi la mahojiano ili kutoa fursa ya kuwasikiliza Wakimbizi hao na kufanya maamuzi sahihi kuhusu hadhi zao kwa kuzingatia sheria za ndani, kikanda na kimataifa.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe Daniel Sillo, akicheza ngoma ya asili ya Kirundi wakati ziara yake katika kambi ya Wakimbizi ya Nduta Wilayani Kibondo Mkoani Kigoma Agosti 7, 2024.

Kauli hiyo imetolewa Agosti 7, 2024 Mkoani Kigoma na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Daniel Sillo, wakati akihitimisha ziara yake na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Maendeleo ya Jamii na Usalama wa Raia wa Burundi, Mhe. Nibona Bonansize katika kambi za wakimbizi za Nyarugusu na Nduta Mkoani humo.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe Daniel Sillo, akizungumza na vyombo vya habari wakati akihitimisha ziara yake katika kambi za Wakimbizi za Nyarugusu na Nduta Mkoani Kigoma Agosti 7, 2024.

Mhe. Sillo alisema Serikali itachukua hatua hiyo endapo Idadi ya Wakimbizi wanaojitokeza kurudi kwao kwa hiari itaendelea kuwa ndogo baada ya mawaziri hao kufanya Mikutano miwili na wakimbizi na kuelezwa hali ya usalama katika nchi yao ya Burundi.

“Urejeaji huu ni wa hiari kama yalivyo makubaliano yetu lakini kama Serikali tunatoa wito na tunasisitiza warudi wakaijenge nchi yao ya Burundi kwani kwa sasa iko salama,”alisisitiza Mhe. Sillo.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Daniel Sillo akizungumza na Wakimbizi waishio katika Kambi ya Nduta, iliyopo Wilayani Kibondo mkoani Kigoma Agosti 7, 2024.

Aidha, alisema Serikali ina mpango mahsusi baada ya muda huo kwenda nyumba kwa nyumba kufanya tathimini ya kila mkimbizi kujua tatizo ni nini, kwanini amekimbia na kwanini anakuwa na mashaka ya kurudi nchini kwao na wakati nchi iko salama.

“Tutafanya tathimini ya kutosha mtu kwa mtu, familia kwa familia na kuhakikisha tunapata sababu za kutosha kwamba kwanini hawataki kurudi nyumbani lakini tunaendelea kuhamasisha kwamba lengo na nia ni kuhakikisha wanarudi salama nyumbani kwao kwenye nchi yao ya asili ya Burundi” Alisema Mhe. Sillo.
Sehemu ya Wakimbizi waishio katika Kambi ya Nduta, iliyopo Wilayani Kibondo, Mkoani Kigoma wakimsikiliza Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Daniel Sillo (hayupo pichani) wakati alipokuwa akizungumza na wakimbizi hao Agosti 7, 2024.

Naye Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Maendeleo ya Jamii na Usalama wa Raia wa Burundi, Mhe. Nibona Bonansize, alisema hali ya kiusalama nchini humo ni salama na shughuli za kimaendeleo zinaendelea vyema hivyo kuwataka kurejea nyumbani kusaidia kulijenga Taifa lao kiuchumi.

“Ifikapo mwaka 2060 tunatarajia kuwa mbali zaidi hivyo hatuna sababu ya Warundi kuendelea kuwa nje ya nchi bali warejee nchini ikiwa ni pamoja na idadi hii kubwa ya Watoto na Vijana ambao ni tegemeo na nguvu kazi ya Taifa”Alisema Mhe. Bonansize.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Daniel Sillo, akipiga ngoma ya asali ya Kirundi na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Maendeleo ya Jamii na Usalama wa Raia wa Burundi, Nibona Bonansize, baada ya kuwasili katika kambi ya Wakimbizi ya Nduta iliyopo Wilayani Kibondo, Mkoani Kigoma Agosti 7, 2024.

Vilevile aliwataka wazazi kuamua kurejea nyumbani ili kuhakikisha watoto wanapata elimu na haki zao za msingi kwani kuendelea kubaki kambini wanazidi kukosa haki zao za kimsingi ikiwa ni pamoja na kupata elimu bora.

Itakumbukwa kuwa kwenye Mkutano wa 24 uliohusisha pande tatu Serikali ya Tanzania, Burundi na UNHCR, uliyofanyika Novemba, 2023 Jijini Dar es Salaam na kuazimiwa kuwa wakimbizi 2,000 wawe wanarejea kwa wiki lengo ambalo halijawahi kufikiwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news