Serikali kukamilisha ujenzi wa vituo vya polisi 77 nchini

MWANZA-Serikali imesema itakamilisha Ujenzi wa Vituo vya Polisi 77 nchini vilivyoanzishwa kwa nguvu za Wananchi lengo likiwa ni kuhakikisha inasogeza karibu huduma hiyo kwa jamii hasa kwa wale wanaoifuta umbali mrefu.Kauli hiyo imetolewa leo Agosti 2, 2024 na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Daniel Sillo katika ziara yake ya kikazi mkoani Mwanza baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Kituo cha Polisi Nyegezi Wilayani Nyamagana kilichoanzishwa kwa nguvu za Wananchi hadi kufikia hatua ya lenta.
Naibu Waziri Sillo, pamoja na mambo mengine amesema Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi itahakikisha inakamilisha Ujenzi wa Vituo vyote 77 nchini vilivyoanzishwa ujenzi wake kwa nguvu za Wananchi kikiwemo Kituo hicho cha Nyegezi.

Amesema katika mwaka wa fedha 2024/25, Serikali itajenga vituo vingine vipya 12 kwenye Kata mbalimbali pamoja na nyumba za Askari wa Jeshi la Polisi kwa kutumia fedha za mfuko wa tuzo na tozo.

"Niuhakikishie Umma kuwa Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani Nchini tunaenda kumalizia hivi Vituo 77 ambavyo vipo kwenye hatua za boma na kama hili boma la Ujenzi wa Kituo cha Polisi Nyegezi lipo kwenye 77 linamaliziwa na kama halipo basi tuanaangalia jinsi ya kuliweka kweli kituo kinahadhi ya kuitwa cha wilaya."
Aidha,Naibu Waziri Sillo, katika ziara yake ametembelea Zahanati ya Jeshi la Polisi Mabatini iliyopo Kata ya Mabatini ambayo imekuwa ikitumiwa na Jeshi la Polisi Jijini Mwanza na Wananchi ambayo kwa sasa inakabiliwa na changamoto ya vifaa tiba pamoja na Wodi ya wakina baba na kuahaidi kuhakikisha inaingizwa kwenye mipango ya maboresho kupitia Wizara hiyo.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Nyamagana Jiji la Mwanza, Mhe. Stanslaus Mabula, amesema Zahanati hiyo ya Mabatini inauhitaji mkubwa wa vifaa tiba na mashine mbalimbali za kufanyia vipimo vya kiafya hivyo ameomba Serikali kupitia Wizara ya Afya na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchini kuhakikisha wanakifanyia marekebisho makubwa maana kinatumika kama Zahanati ya Kanda ya Ziwa.
"Mhe. Naibu Waziri Zahanati hii inatumika kama Zahanati ya Kanda ya Ziwa inatumiwa sana na Maafisa wa Jeshi letu la Polisi pamoja na Wananchi hivyo naomba muitizame kwa jicho la pili inahitaji maboresho na vifaa vya kufanyia huduma Ukanda huu wote hakuna Kituo kingine,"amesema Mhe. Mabula.

Diwani na Mkazi wa Kata ya Nyegezi,Mhe. Edith Mudogo amesema wao kama Wananchi walikuwa na uhitaji mkubwa sana wa Kituo cha Polisi kwa ajili ya kupunguza vitendo vya kiharifu hivyo wametumia nguvu nyingi hasa kufikisha jengo hilo katika hatua ya boma.
Amesema,wanaiomba Serikali iweke fedha ili kuharakisha Ujenzi wa Kituo hicho kukamilika waweze kuondokana na changamoto za kupata huduma za kijamii kama maeneo mengine.

"Tumeanza taratibu kwa kupiga mawe hadi kufikia hatua hii hivyo tunaiomba Serikali ione umuhimu wa kuongeza nguvu zaidi ujenzi ukamilike ili tupate huduma kwenye ukanda huu wa Nyegezi,"amesema Mhe. Mudogo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news