DAR-Serikali ya Tanzania kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina imepokea Gawio la Shilingi Bilioni 4.35 kutoka Shirika linalosimamia Bomba la Mafuta kutoka Tanzania kwenda Zambia (TAZAMA).

Akizungumza katika hafla ya kupokea hundi ya Gawio hilo iliyofanyika leo Agosti 26,2024 jijini Dar es Salaam, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt.Doto Biteko amesema kitendo hicho ni hatua muhimu kwa Tanzania kwani mradi huo una miaka mingi na sasa matunda yanaonekana.

“Mara ya mwisho kutoa gawio kwa serikali ilikuwa miaka mitano iliyopita, na sasa tumepokea fedha hizi, tunajivunia maana badala ya kuja na sababu na visingizio kadha wa kadha lakini mmekuja na fedha, kuna baadhi ya taasisi wanakuja na maneno mengi ya kijanja… unajua kulikuwa na Covid, tatizo la dola lakini nyie hamkuwa hivyo, tunatarajia wakati mwingine kutakuwa na habari njema zaidi,” alisema.
“Naipongeza bodi na uongozi wa Tazama kwanza kwa kufanya jambo hili liwezekane, nataka kuwahakikishia serikali yetu kupitia Wizara ya Nishati tuko kwenye mazungumzo mazuri ya kuongeza uwekezaji kwenye bomba letu la Tazama kama mnavyofahamu tunataka kupanua bomba lililopo kutoka nchi nane hadi 12 na litaanza muda si mrefu ili tusafirishe mafuta mengi kwenda Zambia na baadae kutoka Zambia kwenda nchi za Kongo (DRC) na majirani zetu."
Alisema pia wanakusudia kuanza ujenzi wa bomba jipya la inchi 24 na kwa sasa wapo kwenye hatua mbalimbali za manunuzi nia ni kuona mafuta mengi zaidi yanasafirishwa kwa bomba badala ya malori.



