Serikali yafikisha Elimu ya Fedha Mikumi, yatoa msisitizo kwa watoa huduma ndogo za fedha

NA RAMADHAN KISSIMBA
WF

WATOA huduma ndogo za fedha na vikundi vya kijamii nchini vinavyojihusisha na huduma za mikopo vimetakiwa kuwapatia nakala ya mkataba wananchi wanaowakopesha mikopo.
Afisa Usimamizi wa Fedha kutoka Wizara ya Fedha, Bi. Grace Muiyaza, akiongea na wananchi wa Mikese mkoani Morogoro katika programu ya elimu ya fedha yaliyotolewa kwa wananchi wa Mamlaka ya Mji Mdogo Mikumi.

Akizungumza katika programu ya elimu ya fedha kwa wananchi wa Mji Mdogo wa Mikumi, Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro, Afisa Usimamizi wa Fedha kutoka Idara ya uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha Bi. Grace Muiyanza, alisema kuwa watoa huduma wanatakiwa kutoa mikataba kwa wanaowakopesha kwa mujibu wa sheria iliyowekwa na Benki Kuu ya Tanzania.
Wananchi wa Mji Mdogo wa Mikumi wakimsikiliza mtaalamu kutoka Kampuni ya Uwekezaji ya UTT (UTT-AMIS) Bw. Rahim Mwanga, wakati wa programu ya elimu ya fedha kwa umma iliyotolewa kwa wananchi hao.

Aidha, Bi.Muiyanza alisema mkataba ni mafungamano kati ya pande mbili ya mkopeshaji na mkopaji hivyo ni lazima kila upande uridhie makubaliano hayo kabla ya kuchukua mkopo na kwa kufanya hivyo itasaidia kupunguza changamoto zinazojitokeza wakati wa kurejesha mkopo na pia mkataba utakuwa ndio njia pekee ya kila mmoja kupata haki yake itakapotokea mgongano baina yao.
Afisa Masoko Mwandamizi kutoka Kampuni ya Uwekezaji ya UTT,Bw. Rahim Mwanga akiongea na washiriki wa programu ya elimu ya fedha kwa umma (hawapo pichani) iliyotolewa katika Mji mdogo wa Mikumi mkoani Morogoro.

Pia, Bi. Muiyaza aliwasihi wananchi kabla ya kusaini mkataba wa mkopo ni vizuri kila mmoja akapata nafasi ya kuusoma na kuelewa masharti ya mkataba huo ili usije ukamfunga kwa vipengele ambavyo vitasababisha ugumu wa kurejesha mkopo wake.

‘’Mkataba ni masharti ya pande mbili, hakikisha umeusoma na kuuelewa mkataba, na hata kama ujui kusoma nenda kwa maafisa wa maendeleo ya jamii wakueleweshe masharti yaliyomo kwenye mkataba huo maana ukiamua kusaini bila ya kuuelewa utakuwa umeshakubaliana na masharti na utakuwa umesaini masharti yatakayokuja kukufunga baadae.’’

Awali akifungua mafunzo hayo Afisa Mtendaji wa Mamlaka ya Mji Mdogo Mikumi Bi. Edith Mlay, aliwataka wananchi wa Mikumi kuitumia fursa hiyo ya kujifunza masuala ya fedha ili kuweza kutatua changamoto mbalimbali wanazokutana nazo kutoka kwa baadhi ya watoa huduma za fedha.
Afisa Usimamizi wa Fedha kutoka Wizara ya Fedha, Bi. Grace Muiyaza, akiongea katika kikao kati ya timu ya wataalamu wa masuala ya fedha na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa (hayupo pichani) walipotembelea ofisini hapo kabla ya kuanza kwa program ya elimu ya fedha kwa wananchi wa Kilosa. Pembeni kwa Bi. Grace ni Afisa Mipango kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Masoko na Dhamana Bw.Godfrey Makoi na Afisa Usimamizi wa Fedha kutoka Wizara ya Fedha, Bw. Jackson Mushumba.

Bi. Mlay aliongeza kuwa,elimu ya fedha ni muhimu sana kwa wananchi wa Mikumi kwa sababu mji huo umekusanya makundi muhimu ya kijamii yakiwemo ya wakulima na wafugaji, hivyo elimu hiyo itawasaidia wananchi hao kutumia fursa ya uwekezaji zilizopo katika sekta ya fedha baada ya kuuza mazao yao.

Wizara ya Fedha na washirika wa sekta ya fedha nchini imehitimisha programu maalum ya elimu ya fedha kwa umma kwa Mkoa wa Morogoro ambapo elimu hiyo ilitolewa katika Halmashauri saba (7) ambazo ni Halmashauri ya Morogoro Mjini, Morogoro vijijini, Kilosa, Mvomero, Ifakara, Mlimba na Gairo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news