Serikali yawapongeza wananchi Ifakara kwa kuwa na nidhamu ya mikopo

NA RAMADHAN KISSIMBA
WF Morogoro

MKUU wa Wilaya ya Kilombero, Mhe. Dustan Kyobya amewapongeza wananchi wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara Wilayani Kilombero kwa kuwa na nidhamu na mikopo waliyochukua na kuirejesha kwa wakati.
Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Mhe. Dustan Kyobya, akizungumza na timu ya program ya elimu ya fedha kwa Umma kutoka Wizara ya Fedha na washirika wa sekta ya fedha nchini, Ofisini kwake iliyopo Halmashauri ya Mji wa Ifakara, Wilayani Kilombero kabla ya uzinduzi wa mafunzo ya elimu ya fedha yaliyofanyika katika ukumbi wa chuo cha maendeleo.

Mhe. Kyobya amesema hayo wakati akifungua program maalum ya Elimu ya Fedha kwa Umma inayoendeshwa na Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na washirika mbalimbali wa sekta ya fedha nchini iliyofanyika katika Ukumbi wa Chuo cha Maendeleo – Ifakara, Mkoani Morogoro.
Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, mkoani Morogoro, Mhe. Dustan Kyobya, akizungumza na washiriki wa mafunzo ya elimu ya fedha kutoka katika kata na tarafa mbalimbali za Halmashauri ya Mji wa Ifakara (hawapo pichani) wakati akifungua mafunzo hayo yaliyofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Maendeleo.

‘’Wakina Mama mpo vizuri sana katika kurejesha mikopo mnayochukua na ndio maana uchumi wa wanawake katika mji wa Ifakara unakua kwa kasi ikilinganishwa na vijana ambao wamekuwa na tabia ya kutorejesha mikopo yao kwa wakati’’ alisema Mhe. Kyobya.

Aidha, aliongeza kuwa ili kupata maendeleo ya haraka ni vyema watu wakope kupitia Taasisi zilizoidhinishwa na Wizara ya Fedha kupitia Benki Kuu ya Tanzania, kwa kufanya hivyo wataepuka changamoto mbalimbali zinazotokana na wakopeshaji wasio rasmi ambao wamekuwa wakiwaingiza wananchi kwenye hatari ya kutaifishwa mali zao.
Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Mhe. Dustan Kyobya, akimuelekeza jambo Afisa Usimamizi wa Fedha kutoka Wizara ya Fedha, Bw. Stanley Kibakaya wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya elimu ya fedha yaliyofanyinyika katika ukumbi wa Chuo cha Maendeleo uliopo katika Halmashauri ya Mji wa Ifakara. Pembeni kwa Bw. Kibakaya ni Afisa Sheria Mwandamizi kutoka Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Ramadhani Myonga.

Mhe. Mkuu wa Wilaya aliwataka wananchi wa Halamshauri ya Mji wa Ifakara kuitumia vizuri fursa ya elimu ya fedha waliyoipata ili iwasaidie kutatua changamoto wanazokutana nazo kupitia mikopo hasa ile inayotolewa kwa masharti magumu na mikataba isiyoeleweka inayoandaliwa na baadhi ya watoa huduma wa fedha nchini.

‘’Najua kuwa mnachangomoto kubwa mnayoipata kupitia watoa huduma za fedha wasio waaminifu kwa kuwapa mikataba iliyoandaliwa kwa lugha ya kiingereza, wakati wengi wenu hamfahamu lugha hiyo, na kuna mtoa huduma za fedha mmoja nilishamfukuza Wilayani kwangu kwa kusumbua wananchi na mikopo yake isiyoeleweka," aliongeza Mhe. Kyobya.
Mratibu wa Mifuko na Program za Uwezeshaji, kutoka Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), Bw. Samwel Shikona, akielezea fursa za kuwawezesha wananchi kiuchumi zinazotolewa na Baraza hilo wakati wa program ya elimu ya fedha iliyotolewa na Wataalamu kutoka Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya fedha nchini katika ukumbi wa mikutano wa chuo cha maendeleo uliopo katika Halmashauri ya Mji wa Ifakara.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya elimu ya fedha kutoka katika kata na tarafa mbalimbali za Halmashauri ya Mji wa Ifakara wakifuatilia mada zilizotolewa na watalaamu wa masuala ya fedha katika ukumbi wa Chuo cha Maendeleo.
Kaimu Afisa Maendelo ya Jamii wa Wilaya ya Kilombero akifafanua jambo wakati wa mafunzo ya elimu ya fedha yaliyofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Maendeleo uliopo katika Halmashauri ya Mji wa Ifakara.
Mshiriki wa mafunzo ya elimu ya fedha kutoka katika Halmashauri ya Mji wa Ifakara Bw. Serafin Kazibudi, akichangia mojawapo ya mada iliyotolewa katika mafunzo hayo yaliyofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Maendeleo.

Vilevile Mhe. Kyobya aliipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, kwa kuamua kutoa elimu ya fedha hasa kwa wananchi wa vijijini, na kuongeza kuwa kutokana na fursa nyingi za kilimo zilizopo Kilombero, elimu hiyo itawanufaisha wananchi wa Wilaya hiyo katika kuongeza uzalishaji wa mazo ya kilimo na kukuza Uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

Mhe. Kyobya aliwaagiza Maafisa Maendeleo ya Jamii wa Wilaya ya Kilosa kuhakikisha wanaratibu mafunzo ya aina hiyo yanafanyika mara kwa mara katika kata zote Wilayani Kilombero ii kutatua changamoto zinazowakabili wananchi wa Wilaya hiyo kuhusu mikopo umiza.
Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, mkoani Morogoro, Mhe. Dustan Kyobya akiwa katika picha ya pamoja na waratibu wa mafunzo ya elimu ya fedha, Maafisa wa Maendeleo ya Jamii kutoka Wilaya ya Kilombero na washirika kutoka sekta ya fedha nchini mara baada ya kufungua program maalum ya mafunzo ya elimu ya fedha yaliyofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Maendeleo.(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Fedha).

Program maalum ya elimu ya fedha kwa maeneo ya Mkoa wa Morogoro inalenga kuwahimiza wananchi kujiwekea akiba katika Taasisi rasmi za fedha kama vile benki nk, ili kuweza kuwa na fedha kwa ajili ya shughuli za kilimo badala ya kutumia fedha zote na Kwenda kukopa mikopo umiza wakati wa kilimo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news