Serikali yawashauri raia wa Burundi kurejea nyumbani, kwani Burundi ni salama sasa

KIGOMA-Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Daniel Sillo amewaasa Wakimbizi waishio katika kambi ya Nyarugusu iliyopo Wilayani Kasulu mkoani Kigoma kurudi nchini kwao kwani kwa sasa hali ya kiusalama ni nzuri kulinganisha na hapo awali.
Kauli hiyo ameitoa Agosti 6, 2024 wakati akizungumza na Wakimbizi wa Taifa la Burundi waishio katika kambi ya Nyarugusu huku akiwataka kujiandikisha kwa hiari kurudi nyumbani kwao ili kwenda kujenga Taifa imara.
Mhe. Sillo amesema Serikali inatambua kuwa nchi ya Burundi ina amani na hivyo hawaoni sababu ya kutojiandikisha na kurudi nchini kwao kwa hiari.

“Tunawahamasisha kwa nia njema kuendelea kujiandikisha na kurudi nchini kwenu kwa hiari, ili muweze kuungana na familia na jamaa zenu kwani Burundi ni salama kabisa,”amesema Mhe. Sillo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Huduma kwa Wakimbizi nchini, Sudi Mwakibasi alitumia fursa hiyo kuwaasa Wakimbizi hao kutoshiriki katika vitendo vya siri na vilivyo vya wazi vinavyoashiria uvunjifu wa amani ndani ya kambi na nchi kwa ujumla maana wao ndio mawakala wa usalama katika maeneo wanayoishi.

"Ni vyema mkatambua kuwa ninyi ni sehemu ya jamii ya Taifa la Burundi mnawajibika moja kwa moja na suala la usalama wa kambi na usalama wa nchi ya Tanzania na Burundi kwa ujumla,"amesema.
Awali akisoma taarifa yake Mkuu wa kambi ya Nyarugusu, Siasa Manjenje mbele ya Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Tanzania na Burundi wakati walipotembelea kambi hiyo, amesema hadi kufikia Agosti 6, 2024 kambi ya wakimbizi Nyarugusu ina jumla ya wakimbizi 134,920 kati yao wakimbizi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) 87,190 na kutoka nchini Burundi ni 47,588,”amesema Manjenje.

Amesema katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Agosti, 2024 jumla ya wakimbizi 1655 wamewezeshwa kurejea nchini kwao Burundi kwa hiari ikiwa ni idadi nje ya malengo ya kurejesha wakimbizi 28,000 katika kipindi cha miezi saba.
Naye Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Maendeleo ya Jamii na Usalama wa Raia wa Burundi Brigedia Jenerali, Nibona Bonansize, amesema nchi hiyo inawahitaji wakimbizi wote warudi nyumbani ili kuijenga nchi huku akiishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuwahifadhi ndugu zao kwa muda mrefu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news