Serikali yawataka wafugaji kuanzisha vyama vya Ushirika

PWANI-Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdalla Ulega amewaasa wafugaji nchini kuanzisha na kujiunga na vyama vya Ushirika ili kupata tija katika uzalishaji, utunzaji na uuzaji mazao yatokanayo na mifugo ndani na nje ya nchi.
Ameyasema hayo alipotembelea na kukagua Machinjio ya Union Meat Abattoir Ltd yaliyopo Kata ya Vigwaza Halmashauri ya Chalinze Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani ambapo ameeleza kuwa Ushirika utawapa wafugaji manufaa ya kuinua na kuimarisha uchumi wa mfugaji mmoja mmoja na Taifa Kwa Ujumla.

Kufuatia ombi la kampuni inayomiliki Machinjio hayo ya kupewa maeneo ya kukusanya na kulisha mifugo kabla ya kuingizwa machinjioni, Waziri Ulega ameiagiza kampuni ya Ranchi za Taifa Ltd (NARCO) kutenga eneo kwa ajili hiyo na kuikabidhi kwa kampuni hiyo mapema iwezekanavyo.

"Ninatambua maombi yenu ya kupatiwa eneo, ninaielekeza NARCO itoe eneo hilo haraka iwezekanavyo, apewe mwekezaji kabla ya msimu wa mvua ili aandae na kupanda malisho tayari kwa kupokea mifugo, mkataba na makabidhiano yakamilike mara moja ndani ya mwezi huu wa tisa, kwani huu sio wakati wa danadana, ni wakati wa kuamua," amesema Ulega.

Pia waziri huyo kupitia machinjio hayo amewaasa vijana wanaopata ajira kwenye maeneo ya uwekezaji kufanya kazi kwa uadilifu, uaminifu na bidii kubwa na kuepuka wizi.

Pia,amehimiza mwekezaji wa machinjio hayo kuweka viwango vizuri (gharama za huduma na bei za bidhaa) ili waweze kuwavutia wafanya biashara wengi zaidi wafikishe mifugo yao kuchinjwa hapo.

Mkurugenzi Mtendaji wa machinjio hayo,Mariam Ng'wandu amesema, wametumia Dola za kimarekani Milioni kumi (sawa na shilingi bilioni 26 za kitanzania) kukamilisha awamu ya kwanza ya ujenzi wake na wa Zahanati ya Kijiji cha Vigwaza na kwamba kitakamilika kwa ujenzi wa awamu tatu.

Naye mwakilishi wa mkuu wa mkoa wa Pwani ambaye ni mkuu wa Wilaya ya Kibaha,Nickson Simon amesema kuwa, Serikali imeweka miundombinu wezeshi na rafiki Kwa wawekezaji kama vile huduma za maji, umeme na Barabara ili kurahisisha uwekazaji.

Akiwa katika Kata ya Kwala Kijiji cha Mperamumbi kitongoji cha Msua Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Waziri Ulega amepata fursa ya kujionea uwekezaji wa uchimbaji wa bwawa la kunyweshea mifugo.

Hadi sasa ujenzi wa Bwawa hilo umegharimu kiasi cha shilingi milini 75.23, fedha hizo ni zilizochangwa na wafugaji ambao walitoa kiasi cha shilingi milioni 63.76, mapato ya ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha shilingi milioni 10 na wadau mbalimbali shilingi milioni 1.51.

Kutokana na jitihada hiyo Waziri Ulega ameahidi kuwa Serikali kupitia Wizara yake itatoa shilingi milioni 50 ili kukamilisha ujenzi huo.

Akiwa bwawani hapo, Waziri Ulega amewaasa wafugaji kutojihusisha na migogoro, mifarakano na mapigano kati yao na wakulima kwa sababu zozote zile.

"Ishini kwa amani, na jamii zingine, msifanye vitendo vya uvunjifu wa amani, kaeni mzungumze au nendeni kwa viongozi na vijiji vyote viwe na viongozi wa maridhiano, na hii ndiyo Sera ya Rais Samia Suluhu Hassan, tunahitaji kuvumiliana, kustahimiliana na kuheshimiana hivyo msitumie bakora kuwachapa wakulima," ametahadharisha Ulega.

Wakati huo huo waziri Ulega ametoa mbegu za nyasi za kisasa za malisho ya mifugo pamoja na dawa za kuoshea mifugo.

Kadhalika Waziri Ulega amemtembelea Mohamed Furaha Rangwa ambaye ni mfugaji bora anayefuga kwa njia ya kisasa katika Kijiji cha Gumba Kata ya Gwata ambaye ametumia kiasi cha shilingi milioni 31 kujenga bwawa la maji kwa ajili ya mifugo yake.

Katika taarifa yake mfugaji huyo amesema kuwa awali alitumia kiasi cha shilingi milioni 56.4 kuchimba visima vinne vya maji bila ya mafanikio ndipo akafikia uamuzi wa kjenga bwawa hilo.

Kutokana na hali hiyo, Waziri Ulega ameielekeza Wizara yake kujenga mabwawa maeneo yenye changamoto za upatikanaji wa maji ya visima ili kuokoa fedha za wananchi na akaahidi Wizara yake kujenga josho ndani ya eneo la mfugaji huyo ili liwe msaada kwa wafugaji katika kijiji hicho ambapo pia ametoa mbegu za nyasi za malisho Kwa mfugaji huyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news