Serikali yawezesha wachimbaji wadogo kuaminika kwa taasisi za fedha, CRDB yawajaza mabilioni ya fedha

SHINYANGA-Kutokana na juhudi mbalimbali zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya Madini inaendelea kuziaminisha sekta za fedha kuwa wachimbaji wadogo na wafanyabiashara wa madini nchini wanayo fursa ya kupata mikopo.

Ni kwa ajili ya kuongeza uzalishaji na kuendesha shughuli zao katika mnyororo mzima wa sekta ya madini.
Hayo yamebainishwa leo Agosti 19, 2024 na Waziri wa Madini,Mhe. Anthony Mavunde mkoani Shinyanga katika hafla fupi ya utoaji wa mfano wa hundi ya shilingi bilioni 10 kwa wachimbaji wadogo na wafanyabiashara wa madini ikiwa ni mkopo kutoka Benki ya CRDB.Waziri Mavunde amesema kuwa, mikopo iliyotolewa itasaidia kuikuza na kuiendeleza Sekta ya Madini na hivyo kupelekea kuongeza kwa mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa na uchumi wa nchi.
Aidha,Waziri Mavunde ameipongeza Benki ya CRDB kwa kutoa mkopo wa shilingi bilioni 10 kwa wachimbaji wadogo na watoa huduma na kutumia fursa hiyo kuzitaka benki nyingine pia kuiunga mkono sekta ya madini kupitia utoaji wa mikopo.

Awali, akiwasilisha Ripoti ya Utekelezaji wa Kutoa Huduma za Kifedha kwa wachimbaji wadogo nchini, Afisa Mkuu wa Biashara wa Benki ya CRDB,Boma Raballa amesema, Benki ya CRDB itaendelea kutoa mikopo kwa wachimbaji nchi nzima.
Raballa amesema, lengo ni kuwainua katika mitaji ya kuendesha shughuli za uzalishaji madini nchini.

Mpaka sasa Benki ya CRDB imetoa mikopo ya kiasi cha shilingi bilioni 64 ambapo shilingi bilioni 19 sawa na asilimia 30 zimeelekezwa kwa wachimbaji wadogo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga,Mheshimiwa Anamringi Macha amesema, Mkoa wa Shinyanga ni moja ya mikoa ya kimadini ambao unatambua mchango wa sekta ya madini.
Amesema, katika mwaka wa 2023/2024 ulifikisha asilimia 85 ya ukusanyaji wa maduhuli hivyo upatikanaji wa mikopo kwa wachimbaji wadogo utachochea shughuli za uchimbaji wa madini ambao utasaidia kuongezeka kwa mapato ya serikali.

Naye Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini,Mhe.Masache Kasaka ameipongeza Wizara ya Madini na taasisi zake kwa juhudi mbalimbali inazofanya katika mageuzi makubwa ndani ya sekta ya madini ikiwa ni sehemu ya maelekezo mbalimbali yanayotolewa na kamati ikiwemo hilo la kusimamia upatikanaji wa mikopo kwa wachimbaji wadogo.
Akitoa salamu, Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimba Madini Tanzania (FEMATA), John Wambura Bina amempongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa kwenye sekta ya madini.
Bina amesema, ni uwekezaji ambao umeanza kuleta tija na kuaminika kwa wachimbaji wadogo kukopesheka kwakuwa sasa kuna mashine za uchorongaji zinazosaidia kupata taarifa za awali za uwepo wa madini na hivyo kuwatoa wachumbaji kwenye kuchimba kwa kubahatisha.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news