Shilingi Bilioni 77.9 kuwezesha miradi ya nishati safi ya kupikia nchini

ZANZIBAR-Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imeidhinisha kiasi cha Shilingi Bilioni 77.9 kwa ajili ya kuwezesha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya Nishati Safi ya Kupikia.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Teknolojia za Nishati Jadidifu na Mbadala kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Advera Mwijage hivi karibuni wakati wa Kongamano la Nishati Safi ya Kupikia Kizimkazi Dimbani, Mkoa wa Kusini Unguja.

“Serikali imeidhinisha kiasi cha shilingi bilioni 77.9 kutekeleza zaidi ya miradi tisa ya Nishati Safi ya Kupikia itakayonufaisha Kaya na taasisi mbalimbali za Umma na katika fedha hizo jumla ya shilingi bilioni 16 ni mchango kutoka kwa Wabia wa Maendeleo,” alifafanua Mhandisi Advera.

Akizungumzia miradi itakayotekelezwa, gharama na idadi ya wanufaika alisema ni pamoja na Mradi wa kusambaza majiko banifu wa shilingi Bilioni 16 utakaonufaisha kaya 200,000 na Mradi wa Tsh. Bilioni 10 wa kusambaza Mitungi ya Gesi (LPG) ya kilo 6 utakaonufaisha watanzania wapatao 452,445.

“Tunao pia Mradi wa shilingi bilioni 26.57 sawa na asilimia 76 wa kuwezesha Jeshi la Magereza nchini kuhamia kwenye Nishati Safi ya Kupikia utakaonufaisha maeneo 211 ya Jeshi la Magereza.

"Sambamba na Mradi wa kuwezesha Jeshi la Kujenga Taifa kuhamia kwenye matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia kwenye kambi 22 katika mikoa 14 ambapo mchango wa Serikali ni shilingi bilioni 4.37 ambayo ni sawa na asilimia 76 ya gharama za mradi,” alifafanua.

Mhandisi Advera aliongeza kuwa katika fedha hizo, kiasi cha shilingi bilioni 5.8 kitatumika kutekeleza Mradi wa kusambaza Nishati Safi ya Kupikia katika shule kongwe zipatazo 52 kutoka katika mikoa 18 zenye jumla ya walimu 2,192 na Chuo cha VETA kimoja.

Kwa mujibu wa Mhandisi Advera, miradi mingine itakayonufaika ni Miradi ya kuwezesha utoaji wa elimu kwenye jamii (Tsh. Bilioni 1.86), Mradi wa Ujenzi wa Miundombinu ya kutumia Gesi Asilia katika Mikoa ya Lindi na Mtwara (Tsh. Bilioni 6.82), 

Mradi wa kuongeza uzalishaji wa mkaa mbadala kwa kununua mashine za kutengeneza mkaa (Tsh. Bilioni 3) na Mradi wa kuhamasisha matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia kwa kusambaza mitungi 83,500 (Tsh. Bilioni 3.4).

Aidha, alifafanua kuwa matumizi ya fedha za Nishati Vijijini huzingatia masuala ya kiuchumi na kijamii na hivyo kupelekea baadhi ya miradi kutokulipa kodi na mingine kulipa kodi kutokana na masharti ya kimikataba ya Wabia wa Maendeleo.

Alisema fedha za Nishati Vijijini hutolewa kama ruzuku kwa asilimia 100 lakini wakati mwingine hutolewa kwa mnufaika kuchangia baadhi ya gharama na nyingne kuchangiwa na Serikali na pia ipo miradi ambayo inapata mikopo yenye riba nafuu kutoka REA.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news