DAR-Armee Patriotique Rwandaise (APR FC) kutoka Kigali nchini Rwanda imechapwa mabao 2-0 na Klabu ya Simba ya jijini Dar es Salaam,Tanzania.
Ni kupitia mchezo wa kirafiki wa kilele cha Simba Day dhidi ya APR uliopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa ndani ya Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar Es Salaam.
Katika mchezo huo,mlinda mlango Ally Salim wa Simba alishindwa kuendelea na mchezo na kufanyiwa mabadiliko dakika ya 31 huku nafasi yake ikichukuliwa na Mousa Camara baada ya kupata maumivu.
Mshambuliaji Steven Mukwala alikosa mkwaju wa penati dakika ya 44 baada ya kiungo mshambuliaji, Joshua Mutale kufanyiwa madhambi ndani ya 18.
Aidha,wakati timu hiyo imerejea katika dakika 45 za kipindi cha pili kocha Fadlu Davids alifanya mabadiliko ya kuwatoa Mzamiru Yassin, Fabrice Ngoma, Shomari Kapombe na Awesu Awesu na kuwaingiza Debora Fernandes, Augustine Okajepha, Kelvin Kijili na Edwin Balua.
Debora Fernandes aliwapatia Simba SC bao la kwanza dakika ya 46 kwa shuti kali nje ya 18 baada ya kumalizia pasi ya Mutale.
Dakika ya 57 kocha Fadlu alifanya mabadiliko ya kumtoa mshambuliaji Steven Mukwala na kumuingiza Valentino Mashaka.
Edwin Balua aliwapatia bao la pili kwa mpira wa adhabu uliotinga wavuni moja kwa moja dakika ya 66 baada ya mlinzi wa kulia Kelvin Kijili kufanyiwa madhambi nje ya 18.
Dakika ya 70 kocha Fadlu alifanya mabadiliko mengine ya kuwatoa Mutale, Zimbwe Jr, Jean Charles Ahoua, Karaboue Chamou na Che Fondoh Malone na kuwaingiza Kibu Denis, Valentine Nouma, Omary Omary, Abdulrazack Hamza na Hussein Kazi.
Vile vike, dakika ya 87 kocha Fadlu alifanya mabadiliko ya kuwatoa Mousa Camara, Valentino Mashaka, Omary Omary na kuwaingiza Hussein Abel, Ladaki Chasambi na David Kameta (Duchu).
Kupitia tamasha hilo ambalo lilitawaliwa na burudani za kutosha, pia mashabiki walifurika kila kona huku wachezaji wapya wakitambulishwa.